• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 22, 2018

  CHILUNDA AZUNGUMZIA NAFASI YA KWANZA KUCHEZA TENERIFE: HUU NI MWANZO MZURI KWANGU

  Na Mwandishi Wetu, TARRAGONA
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda amesema amefurahia kupewa nafasi na timu yake mpya, CD Tenerife katika mchezo wa kwanza wa Ligi Daraja la Kwanza Hispania, Segunda.
  Chiliunda amesema kwamba japo zilikuwa dakika chache mno, kwake ulikuwa mwanzo mzuri tosha na sasa anaelekeza nguvu zake kwenye kujibidiisha zaidi ilia pate nafasi zaidi na hatimaye awe mchezaji muhimu.  
  “Kwangu ni mwanzo mzuri sana. Kupewa nafasi hapa katika mechi ya kwanza kabisa, haijalishi kwa muda gani. Ni nafasi nzuri inayonifungulia milango,”amesema.
  Chilunda aliingia dakika 10 za mwisho Jumatatu, CD Tenerife ikilazimisha sare ya 1-1 ugenini na Gimnastic katika mchezo wa Segunda.

  Shaaban Iddi Chilunda amefurahia mwanzo mzuri CD Tenerife katika Segunda 

  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Nou Estadi de Tarragona, Chilunda aliingia uwanjani dakika ya 86 kwenda kuchukua nafasi ya kiungo Mserbia, Filip Malbasic wakati huo Tenerife ikiwa nyuma kwa 1-0, baada ya Fali Jimenez kutangulia kuifungia Gimnastic dakika ya 10 akimaliziai pasi ya David Rocha. 
  Lakini Chilunda akiwa uwanjani ndani ya dakika 10 za mwisho pamoja na nne za nyongeza, Tenerife ikafanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya mwisho, mfungaji akiwa beki Muargentina, Lucas Elio Aveldano akimalizia pasi ya Samuel Geoffroy Camille.  
  Chilunda amejiunga na CD Tenerife mwezi huu akitokea Azam FC ya Tanzania kwa mkopo wa miaka miwili.
  Na huko amekutana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Azam FC ambao wote wameibuliwa katika akademi ya timu ya Chamazi, Farid Mussa Malik ambaye anaingia mwaka wa pili wa Hispania. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHILUNDA AZUNGUMZIA NAFASI YA KWANZA KUCHEZA TENERIFE: HUU NI MWANZO MZURI KWANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top