• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 24, 2018

  CHILUNDA NDANI KIKOSI CHA TENERIFE KINACHOIFUATA ALMERIA MECHI YA SEGUNDA JUMAPILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda amejumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 19 cha CD Tenerife kinachosafiri kwa mchezo wa ugenini Ligi Daraja la Kwanza Hispania, Segunda dhidi ya Almeria Jumapili.
  Tenerife imetaja mapema tu kikosi chake kamili kwa ajili ya mchezo huo wa Segunda unaotarajiwa kufanyika Jumapili, huku Chilunda akijumuishwa.
  Na hiyo ni baada ya chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Chilunda kutokea benchi usiku wa Jumatatu wiki hii kwenda kumalizia dakika 10, CD Tenerife ikilazimisha sare ya 1-1 ugenini pia na Gimnastic katika Segunda.

  Shaaban Iddi Chilunda amejumuishwa kwenye kikosi cha CD Tenerife kinachoifuata Almeria Jumapili

  Huo ndiyo ulikuwa mchezo wa kwanza kabisa kwa Chilunda baada ya kujiunga na CD Tenerife mapema mwezi huu akitokea Azam FC kwa mkopo wa miaka miwili.
  Na katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Nou Estadi de Tarragona, Chilunda aliingia uwanjani dakika ya 86 kwenda kuchukua nafasi ya kiungo Mserbia, Filip Malbasic wakati huo Tenerife ikiwa nyuma kwa 1-0, baada ya Fali Jimenez kutangulia kuifungia Gimnastic dakika ya 10 akimaliziai pasi ya David Rocha. 
  Lakini Chilunda akiwa uwanjani ndani ya dakika 10 za mwisho pamoja na nne za nyongeza, Tenerife ikafanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya mwisho, mfungaji akiwa beki Muargentina, Lucas Elio Aveldano akimalizia pasi ya Samuel Geoffroy Camille.  
  Mchezaji mwingine chipukizi wa Tanzania, Farid Mussa yupo Tenerife pia, lakini yeye bado anachezea timu ya wachezaji wa akiba ambako pia anafanya vizuri kukiwa na matarajio ya kupandishwa kikosi cha kwanza wakati wowote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHILUNDA NDANI KIKOSI CHA TENERIFE KINACHOIFUATA ALMERIA MECHI YA SEGUNDA JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top