• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 26, 2018

  SAMATTA AENDELEZA MOTO WA MABAO KRC GENK IKIPIGA MTU MABAO 3-2 LIGI YA UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ametokea benchi na kuifungia timu yake, KRC Genk ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Waasland Beveren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena.
  Samatta aliingia uwanjani dakika ya 58 kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mbelgiji, Zinho Gano na ikamchukua dakika 20 tu kuifungia bao Genk akimalizia pasi ya kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy.
  Kabla ya kutoka, Gano alimsetia mshambuliaji Mkosovo mzaliwa wa Ujerumani, Edon Zhegrova kuifungia Genk bao la kwanza dakika ya 20 na bao lingine la timu hiyo limefungwa na mshambuliaji mwingine Mbelgiji, Leandro Trossard dakika ya 89.

  Mbwana Samatta ametokea benchi na kuifungia KRC Genk ikishinda 3-2 dhidi ya Waasland Beveren Ligi ya Ubelgiji

  Mabao yote ya Waasland Beveren yamefungwa na kiungo Mghana, Nana Opoku Ampomah dakika za 66 na 75 na kwa matokeo hayo sasa Genk inapanda kileleni, ikifikisha pointi 13 baada ya mechi tano, ikiwa mbele ya Club Brugge yenye pointi 13 pia, Anderlecht pointi 12 na Standard Liege pointi 11 baada y azote kucheza mechi tano tano pia.
  Kikosi cha KRC Genk: Vukovic, Nastic, Dewaest, Aidoo, Maehle, Heynen/Malinovskyi dk74, Seck, Pozuelo, Paintsil, Zhegrova/Trossard dk67 na Gano/Samatta dk58.
  Waasland Beveren: Roef, Massop, Boljevic, Forte/Ndao dk45, Jubitana/Van Damme dk76, Keita, Ampomah, Caufriez, Abdullah/Badibanga dk63, Vukotic na Schryvers.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AENDELEZA MOTO WA MABAO KRC GENK IKIPIGA MTU MABAO 3-2 LIGI YA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top