• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 21, 2018

  PIGO YANGA SC; JUMA MAHADHI AUMIA GOTI NA ATAKUWA NJE KWA WIKI MBILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa Yanga SC, Juma Mahadhi atakuwa nje kwa wiki mbili baada ya kuumia Jumapili katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo ambao Yanga SC ilishinda 2-1, Mahadhi aliingia uwanjani mwanzoni tu mwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Pius Buswita, lakini akaumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na Ibrahim Ajib. 
  Taarifa ya Yanga SC leo imesema; “Juma Mahadhi atakuwa nje kwa wiki mbili kupisha majeraha ya goti aliyopata kwenye mchezo dhidi ya USM Alger,”.

  Juma Mahadhi atakuwa nje kwa wiki mbili baada ya kuumia Jumapili Yanga ikimenyana na USM Alger Uwanja wa Taifa

  Baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya USM Alger, mabao yake yakifungwa na Deus Kaseke na Mkongo Eritier Makambo, Yanga watarudi uwanjani Alhamisi kumenyana na Mtibwa Sugar ya Morogoro, huo ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu.
  Kwa ujumla, Ligi Kuu inatarajiwa kuanza kesho; Simba SC ikiwakaribisha Tanzania Prisons kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Uhuru, Ruvu Shooting na Ndanda FC Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Alliance FC na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Coastal Union na Lipuli FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Kagera Sugar na Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, zote zikianza Saa 10:00.
  Ligi hiyo itaendelea Alhamisi na mbali na Yanga na Mtibwa, JKT Tanzania watamenyana na KMC kuanzia Saa 8:00 mchana Uwanja wa Meja Isamuhuyo, Stand United na African Lyon Saa 10:00 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na Azam FC na Mbeya City kuanzia Saa 2:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PIGO YANGA SC; JUMA MAHADHI AUMIA GOTI NA ATAKUWA NJE KWA WIKI MBILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top