• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 27, 2018

  KAGERE AFUNGA MABAO MAWILI SIMBA SC YAIPIGA 2-0 MBEYA CITY...BOBAN ATIKISA NYAVU KIRUMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere ameendelea kuonyesha umuhimu wake ndani ya kikosi cha Simba SC kufuatia leo kufunga mabao yote, timu hiyo ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Sasa pointi zote sita za SImba SC katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu zimetoka kwenye himaya ya Kagere aliyejiunga na timu hiyo Julai mwaka huu akitokea Gor Mahia ya Kenya, kufuatia kufunga pia bao pekee katika ushindi wa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumatano dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Taifa pia.
  Tofauti na mchezo wa kwanza alifunga kwa guu lake la kulia, leo Kagere amefunga mabao yote kwa kichwa la kwanza dakika ya 11 akimalizia krosi ya kiungo Shiza Kichuya na la pili dakika ya 45 na ushei akimalizia krosi ya beki Mghana, Asante Kwasi.

  Nahodha John Bocco akiwa amemdandia mgongoni Meddie Kagere baada ya kufunga bao la pili leo. Kulia ni mtoa pasi ya bao hilo, Asante Kwasi

  Simba SC ikiwa chini ya kocha wake mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems kwa mara nyingine leo imecheza soka maridadi na kudhihirisha ubora wa kikosi chake pamoja na kuendelea kumkosa mshambuliaji wake tegemeo, Mganda Emmanuel Okwi ambaye ni majeruhi.
  Mbeya City baada ya makosa yaliyoipa Simba SC mabao mawili ya mapema, kipindi cha pili walibadilika na kuanza kucheza kwa uwiano mzuri wa kuzuia na kushambulia, lakini tu wakakosa bahati ya kufunga.
  Pamoja na Simba SC kumpoteza kipa wake namba moja, Aishi Manula aliyeumia mwanzoni mwa kipindi cha pili, mlinda mlango mdogo aliyepandishwa kutoka timu ya vijana, Ally Salim akaenda kufanya nzuri na kuwazuia MCC kupata bao.
  Katika mchezo uliotangulia wa Ligi Kuu leo, Alliance FC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na African Lyon ya Dar es Salaam Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Lyon ilitangulia kwa bao la kiungo mshambuliaji, mkongwe Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya tisa kabla ya Mnigeria, Michael Chinedu kuisawazishia Alliance FC dakika ya 90 na ushei.
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu unaendelea hivi sasa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam kati ya wenyeji, Azam FC na Ndanda FC ya Mtwara.  
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula/Ally Salim dk53, Shomari Kapombe, Asante Kwasi, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, James Kotei, Hassan Dilunga/Said Ndemla dk72, Meddie Kagere, John Bocco/Adam Salamba dk82 na Shiza Kichuya.
  Mbeya City; Owen Chaima, John Kabanda, Mpoki Mwakinyuki, Erick Kyaruzi, Ibrahim Ndunguli, Majaliwa Shaaban, Mohammed Kapenta, Medson Mwakatundu/Suleiman Ibrahim dk86, Chunga Said, Bakari Masoud/Iddi Suleiman ‘Nado’ dk70 na Eliud Ambokile.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGERE AFUNGA MABAO MAWILI SIMBA SC YAIPIGA 2-0 MBEYA CITY...BOBAN ATIKISA NYAVU KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top