• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 24, 2018

  SIMON MSUVA: MWAKA MMOJA WA KUCHEZA MOROCCO UMEBADILI MENGI KATIKA MAISHA YANGU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWEZI huu kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva ameuanza mwaka wa pili wa maisha yake ya kucheza Morocco, kufuatia kujiunga na Difaa Hassan El- Jadidi akitokea Yanga SC ya nyumbani, Tanzania.
  Bin Zubeiry Sports – Online imefanya mahojiano kwa simu na mchezaji huyo mwenye kasi uwanjani juu ya mwaka wake mmoja wa kucheza klabu ya mji wa El Jadida, Mazghan nchini Morocco na mkakati wake kuelekea mwaka wa pili. Endelea.   

  Bin Zubeiry Sports – Online: Hongera kwa kutimiza mwaka mmoja tangu uhamie Morocco.
  Simon Msuva: Asante sana kaka
  Bin Zubeiry Sports – Online: Kwako ilikuwa safari ya aina gani mwaka huu wa kwanza wa kucheza nje ya nyumbani?
  Simon Msuva: Ilikuwa ngumu kidogo, kwanza kubadilisha mazingira na kujifunza mpira wa proffessional na la mwsho nimefurahi kusogea kwenda mahali pengine
  Bin Zubeiry Sports – Online: Siku za mwanzoni hali ilikuwaje, mabadiliko ya nchi, watu, mazingira, vyakula, lugha na mengine?
  Simon Msuva: Ilikuwa ngumu sana kuzoea, maana ilikuwa ni mwanzo. Kila kitu kilikuwa kipya kwangu, lakini kwa sababu nimekuja kutafuta maisha, ilibidi nizoee tu kwa haraka
  Bin Zubeiry Sports – Online: Kuna utaratibu maalum Difaa kwa wachezaji wa kigeni wanapojiunga na timu, hususan ambao hawajui lugha zinazotumika huko?
  Simon Msuva: Ndiyo, kwa mfano mimi nilipewa mwalimu wa saikolojia ambaye pia ni mwalimu wa Chuo Kikuu huku ndiye amekuwa ananisaidia juu ya kila kinachoendelea kwenye timu. Yeye anaongea Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu. 
  Bin Zubeiry Sports – Online: Kuwasiliana na wachezaji wenzako wanaoongea Kiarabu pekee ilikuwaje?
  Simon Msuva: Wapo wachezaji wenzangu wawili wanajua kidogo Kiingereza pia walinisaidia, Ila sasa maneno ya Kiarabu ya uwanjani nayajua
  Bin Zubeiry Sports – Online: Akina nani hao wachezajj wawili?
  Simon Msuva: Tarik Astat na Yahaya Firaly
  Bin Zubeiry Sports – Online: Ilikuchukua muda gani kuzoea na kuanza kujisikia upo nyumbani?
  Simon Msuva: Miezi mitatu hadi minne hivi
  Simon Msuva akiwaongoza wachezaji wenzake kuingia uwanjani
  Simon Msuva akiwa mazoezini na wachezaji wenzake w Difaa Hassan El Jadidi

  Bin Zubeiry Sports – Online: Kuna tofauti kiasi gani mazingira uliyokuwa unachezea nyumbani na huko 
  Simon Msuva: Tofauti ipo na ni kubwa kaka, huku wenzetu wamepiga hatua na wamewekeza sana katika michezo. Hakuna mzaha huku. Huku ni kama Ulaya tu. 
  Bin Zubeiry Sports – Online: Yamekusaidia kiasi gani wewe binafsi? 
  Simon Msuva: Kiasi kikubwa mno, nimekuwa mchezaji ninayejielewa zaidi ya ilivyokuwa nyumbani, ninaishi kama professional kweli. Nyumbani mchezaji ukimaliza mazoezi wakati mwingine unaweza kuzua safari kwenda popote, lakini huku baada ya mazoezi ni kupumzika vya kutosha. Ninapata muda mwingi wa kupumzka na muda mwingi wa mazoezi binafsi. Ukizingatia kambini tunaingia siku moja tu kabla ya mechi.
  Bin Zubeiry Sports – Online: Uwanja mnaoutumia kwa mechi zenu za nyumbani (Ben Ahmed El Abdi) ndiyo wa mazoezi pia? 
  Simon Msuva: Viwanja wanavyo vitatu, viwili vya nyasi za kawaida na mmoja wa nyasi bandia
  Bin Zubeiry Sports – Online: Kuna tofauti yoyote ya ufundishaji kutoka ulivyokuwa unafundishwa hapa nyumbani na huko? 
  Simon Msuva: Mafundisho hamna tofauti sana, sema huku nimekutana na mfumo tofauti na niliokuwa nacheza Yanga na nafasi ninayocheza ni nyingne pia
  Bin Zubeiry Sports – Online: Hebu tueleze hizo tofauti
  Simon Msuva: Huko nilikuwa nacheza kama winga katika mfumo wa 4-4-2, lakini huku natumika kama mshambuliaji (namba 10) katika mfumo wa 4-3-3
  Bin Zubeiry Sports – Online: Ligi ya Morocco ukilinganisha na ya Tanzania kuna tofauti gani?
  Simon Msuva: Tofauti ni kubwa mno kaka, kama nilivyokuambia huku wamepiga hatua mno, Ligi yao ni bora, timu zote bora, viwanja vyote bora, miundombinu bora, mashabiki wanasapoti timu na wachezaji wao. Maslahi ni bora. Na wachezaji wengi wanaotoka hapa wanakwenda kucheza Hispania na Ufaransa
  Bin Zubeiry Sports – Online: Katika mwaka mmoja umefunga mabao mangapi katika mashindano yote?
  Simon Msuva: Nimefunga mabao 22 kwenye mashindano tu, nikijumlisha na ya kwenye mechi za kirafiki yanaweza kufika 40. Katika Ligi peke yake nimefunga mabao 11, Kombe la Mfalme mabao manne, Ligi ya Mabingwa Afrika mabao saba.
  Bin Zubeiry Sports – Online: Na umetengeneza nafasi ngapi jumla za wengine kufunga?
  Simon Msuva: Jumla nafasi 17, lakini kwenye mashindano tu. Nikiongeza na za kwenye mechi za kirafiki zitazidi mno
  Bin Zubeiry Sports – Online: Ukiwa huko unaishi wapi?
  Simon Msuva: Naishi kwangu, nimepewa nyumba kubwa ipo karibu na Uwanja, natembea tu kwenda mazoezini. 
  Bin Zubeiry Sports – Online: Kumekuwa na habari au tetesi tuseme za kutakiwa Hispania, unajua lolote?
  Simon Msuva: Ni kweli zipo, lakini naomba kwa sasa nisizungumzie hizo habari hadi hapo mambo yatakapokamilika.
  Bin Zubeiry Sports – Online: Tukumbushe ulisaini mkataba wa miaka mingapi Jadida?
  Simon Msuva: Nilisaini mkataba wa miaka mitatu na sasa ninauanza mwaka wangu wa pili
  Bin Zubeiry Sports – Online: Umesikia habari za kocha mpya Taifa Stars?
  Simon Msuva: Ndiyo, kocha wetu mpya ni Emmanuel Amunike, gwiji wa Nigeria 
  Bin Zubeiry Sports – Online: Umepokeaje uteuzi wake?
  Simon Msuva: Vizuri tu, nasi wachezaji tunaahidi tutampa ushirikiano mzuri ili tufanikiwe
  Bin Zubeiry Sports – Online: Kumbukumbu gani nzuri zaidi katika kucheza kwako Yanga?
  Simon Msuva: Tulivyochukua ubingwa (Ligi Kuu) mara tatu mfululizo
  Bin Zubeiry Sports – Online: Na kumbukumbu mbaya?
  Simon Msuva: Yanga ni timu yangu, imenilea na kunifikisha hapa, kumbukumbu nyingi ni nzuri, sikumbuki kitu kibaya, labda tu niseme nilikuwa sipendezewi na tabia ya mashabiki kumtukana mchezaji.
  Bin Zubeiry Sports – Online: matarajio yako ya baadaye?
  Simon Msuva: Kufika mbali zaidi ya hapa nilipo
  Bin Zubeiry Sports – Online: Mchezaji gani unampenda zaidi duniani?
  Simon Msuva: Sadio Mane na Cristiano Ronaldo
  Bin Zubeiry Sports – Online: wewe ni mpenzi wa klabu gani Ulaya?
  Simon Msuva: Manchester United
  Bin Zubeiry Sports – Online: Nyumbani?
  Simon Msuva: Nyumbani unauliza tena? Mpenzi wa timu yangu iliyonifikisha hapa na nimeendelea kuwa nayo karibu, wakati wote nikirudi nyumbani lazima niwatembelee wenzangu mazoezini. Tulikutana Algeria wote tumekwenda kwa mechi za ugenini za CAF, nilikwenda kuwatembelea hotelini. Hivyo. 
  Bin Zubeiry Sports – Online: Ukikutana na Mheshimwa Rais Dk. John Pombe Magufuli utamuambia nini kwa maslahi ya michezo nchini?
  Simon Msuva: Serikali ijikite kwenye kusaidia kuinua michezo nchini, ni ajira kubwa kwa vijana wengi. Tukifanikiwa kuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje, wataitangaza sana nchi yetu na kuwavutia watalii kuja kwa wingi zaidi. Nafikiri inatosha kaka, nataka kuwahi mazoezini.
  Bin Zubeiry Sports – Online: Asante. Ninashukuru sana kwa muda wako na nikutakie kila la heri, Mungu akujaalie utimize ndoto zako.
  Simon Msuva: Amin, nawe pia kazi njema kaka. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMON MSUVA: MWAKA MMOJA WA KUCHEZA MOROCCO UMEBADILI MENGI KATIKA MAISHA YANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top