• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 30, 2018

  ATHUMANI CHINA AUNGA MKONO AKINA KAPOMBE KUFUKUZWA TAIFA STARS…LAKINI AMTOLEA UVIVU RAIS KARIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Athumani Abdallah ‘China’ ameunga mkono kitendo cha kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike kuwafukuza wachezaji sita wa Simba SC na mmoja wa Yanga SC kwa utovu wa nidhamu.
  Mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na mshambuliaji na Nahodha, John Bocco wa Simba SC pamoja na kiungo wa Yanga, Feisal Salum wameenguliwa Taifa Stars kwa utovu wa nidhamu.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka London, England anapoishi, China mchezaji wa zamani wa timu zote, Simba na Yanga amesema kwamba masuala ya nidhamu na kufuata utaratibu ni muhimu mno yakazingatiwa katika timu ya taifa.

  Shomari Kapombe ni miongoni mwa wachezaji saba waliofukuzwa Taifa Stars

  “Mimi napingana mno na viongozi wetu wa soka wa sasa, tena kwa mambo mengi sana. Lakini katika hili nawaunga mkono, hatua iliyochukuliwa ni sawa kabisa. Lazima wachezaji wetu wa sasa wabadilike, wawe na nidhamu,”amesema.
  China amesema ifike wakati mchezaji anapoitwa timu ya taifa aheshimu wito na kuzingatia muda bila kutoa visingizio ndipo hata mafaniko yataanza kupatikana.
  “Hatutakiwi kwa namna yoyote kuwatetea wachezaji hawa katika hili. Wamekosea. Kama walipata taarifa na wakapigiwa hadi simu, walipaswa kuripoti kambini kama walivyotakiwa. Hatua hii waliyochukuliwa wazi litakuwa fundisho kwao na kwa wengine,”amesema.       
  Pamoja na hayo, China amesema kwamba anasikitishwa mno na dharau za Rais wa sasa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kusema kwamba Tanzania ina watu wawili tu wa maana nje, ambao ni kocha Ammy Ninje na mchezaji Mbwana Samatta.
  “Hizi ni dharau kubwa sana. Watanzania wengi tupo nje na tunafanya mambo makubwa, tuna uwezo mkubwa. Ukiondoa mimi wapo akina Said Jonh, Hilal Hemed, Hussein Mwakuruzo, Hussein Marsha wote sisi kutuona hatuna maana ni dharau kubwa sana. Mimi bado ninazo zile clip zake anatukandia sasa, roho inaniuma kweli,”amesema China. 
  Athumani China ameunga mkono kocha Emmanuel Amunike kuwafukuza wachezaji Taifa Stars 

  Athumani Abdallah ‘China’ (katikati) akiwa na wachezaji wenzake wa Taifa Stars mwaka 1991, Sanifu Lazaro na David Mwakalebela na George Masatu na Hussein Marsha (kushoto) 

  Baada ya kuwaondoa Kapombe, Nyoni, Mkude, Kichuya, Dilunga, Bocco na Feisal katika kikosi kinachojiandaa na mechi dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, Amunike  amewachukua mabeki, Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli FC ya Iringa, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, David Mwantika, viungo Frank Domayo wa Azam FC, Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato, wote wa Mtibwa Sugar. 
  Taifa Stars iliingia kambini juzi katika hoteli ya Sea Scape, eneo la Kunduchi mjini Dar es Salaam na itakuwa inafanya mazoezi Uwanja wa Boko Veterani.
  Wachezaji walioripoti kambini hadi sasa pamoja na walioongezwa ni makipa Aishi Manula wa Simba SC na Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, mabeki ni Aggrey Morris, viungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Yahya Zayed wa Azam FC.
  Wachezaji wa Yanga SC, kipa Benno Kakolanya, mabeki Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo Feisal Salum ambao wapo na timu yao mjini Kigali, Rwanda ambako jana ilifungwa 1-0 na wenyeji, Rayon Sport katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika watajiunga na timu wakirejea kuanzia jioni ya leo.
  Nyota wanaocheza nje wanatarajiwa kuwasili kuanzia Septemba 1 ambao ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Himid Mao wa Petrojet FC ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida, Morocco, Farid Mussa, Shaaba Iddi wa CD Tenerife  ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, Emmanuel Ulimwengu wa El HIlal ya Sudan) na Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.
  Amunike aliyesaini mkataba wa kufundisha Taifa Stars mapema mwezi huu, ambaye anasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na Mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, baada ya mechi na Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, atawafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ATHUMANI CHINA AUNGA MKONO AKINA KAPOMBE KUFUKUZWA TAIFA STARS…LAKINI AMTOLEA UVIVU RAIS KARIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top