• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 29, 2018

  NYOTA SIMBA SC WAONDOLEWA TAIFA STARS KWA UTOVU WA NIDHAMU, AMUNIKE AWAITA NGALEMA, KONGWE NA KIHIMBWA KUZIBA NAFASI ZAO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI sita wa Simba SC, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na mshambuliaji na Nahodha, John Bocco wameenguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachojiandaa na mechi dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala kwa utovu wa nidhamu.
  Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike amechukua hatua hiyo baada ya wachezaji hao pamoja na Feisal Salum wa Yanga SC kwa kushindwa kuripoti kambini jana, hoteli ya Sea Scape, eneo la Kunduchi mjini Dar es Salaam bila taarifa yoyote, huku mwenzao, kipa, Aishi Salum Manula pekee akiripoti.
  Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau amesema mbali na wachezaji hao viongozi wa Simba, Hamisi Kisiwa na Meneja Richard Robert watapelekwa katika Kamati ya Maadili Jumamosi kwa hatua zaidi.
  Badala yake, Amunike winga wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, amewachukua mabeki, Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli FC ya Iringa, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, David Mwantika, viungo Frank Domayo wa Azam FC, Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato, wote wa Mtibwa Sugar. 

  Wachezaji walioripoti kambini hadi sasa ukiondoa walioongezwa ni makipa Aishi Manula wa Simba SC na Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, mabeki ni Aggrey Morris, viungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Yahya Zayed wa Azam FC.
  Wachezaji wa Yanga SC, kipa Benno Kakolanya, mabeki Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo Feisal Salum ambao wapo na timu yao mjini Kigali, Rwanda ambako leo wanamenyana na wenyeji, Rayon Sport katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika watajiunga na timu wakirejea kuanzia Iiumaa.
  Nyota wanaocheza nje wanatarajiwa kuwasili kuanzia Septemba 1 ambao ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Himid Mao wa Petrojet FC ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida, Morocco, Farid Mussa, Shaaba Iddi wa CD Tenerife  ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, Emmanuel Ulimwengu wa El HIlal ya Sudan) na Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.
  Amunike aliyesaini mkataba wa kufundisha Taifa Stars mapema mwezi huu, ambaye anasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na Mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, baada ya mechi na Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, atawafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NYOTA SIMBA SC WAONDOLEWA TAIFA STARS KWA UTOVU WA NIDHAMU, AMUNIKE AWAITA NGALEMA, KONGWE NA KIHIMBWA KUZIBA NAFASI ZAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top