• HABARI MPYA

    Monday, August 27, 2018

    RATIBA LIGI KUU YAPANGULIWA TENA, MECHI ZA AZAM, SIMBA NA YANGA ZAAHIRISHWA HADI ‘MAJAALIWA’

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MECHI tatu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara za vigogo, Azam FC, Simba na Yanga SC zilizokuwa zifanyike mapema mwezi ujao zimesogezwa mbele hadi hapo itakapotangazwa baadaye.
    Taarifa za ndani kutoka Bodi ya Ligi zimesema kwamba sababu za kuahirishwa kwa michezo hiyo ni idadi kubwa ya wachezaji wa klabu hizo kuitwa katika timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya wenyeji, Uganda Septemba 8 mjini Kampala.
    Mechi hizo ni za Septemba 1, kati ya Azam FC na Ruvu Shooting ya Pwania Uwanja wa Axam Complex, Chamazi na Simba SC dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na ule wa Septemba 2 kati ya Mwadui FC na Yanga SC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

    Haya ni mabadiliko ya pili ya Ratiba ya Ligi Kuu ndani ya wiki mbili za mwanzo tangu ianze, baada ya mchezo kati ya Simba SC na Mbeya City uliokuwa ufanyike Jumamosi kusogezwa mbele hadi leo jioni. 
    Wachezaji wa Simba SC waliopo Taifa Stars ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe na Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya na Hassan Dilunga na mshambuliaji John Bocco, Yanga SC kipa Benno Kakolanya, mabeki Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo Feisal Salum wakati wa Azam FC ni beki ni Aggrey Morris na mshambuliaji Yahya Zayed.
    Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RATIBA LIGI KUU YAPANGULIWA TENA, MECHI ZA AZAM, SIMBA NA YANGA ZAAHIRISHWA HADI ‘MAJAALIWA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top