• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 27, 2018

  AZAM FC YAENDELEZA UBABE LIGI KUU, YAICHAPA NDANDA FC 3-0 KUTINYU MAWILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imepata ushindi wa pili mfululizo katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ndanda FC mabao 3-0 usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo, viungo washambuliaji Tafadzwa Kutinyu aliyefunga mawili na Joseph Mahundi moja.
  Kutinyu alifunga bao la kwanza kwa penalti dakika ya 41 kufuatia beki wa Ndanda FC, Malika Ndeule kuunawa mpira na la pili dakika ya 60 baada ya kuikuta krosi ya Mzimbabwe mwenzake, beki Bruce Kangwa na kuwapangua walinzi kabla ya kufumua shuti lililojaa nyavuni.

  Tafadzwa Kutinyu akiifungia Azam FC bao la kwanza kwa penalti leo 

  Kiungo wa zamani wa Coastal Union na Mbeya City, Joseph Mahundi akakamilisha shangwe za mabao za Azam FC kwa kufunga bao la tatu dakika ya 78 akimalizia pasi ya Daniel Lyanga kufuatia kazi nzuri ya kiungo Frank Domayo.
  Azam FC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao ikiwa inalingana kwa pointi na mabingwa watetezi, Simba SC ambao jioni ya leo waliifunga 2-0 Mbeya City Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya Meddie Kagere kipindi cha kwanza.
  Mchezo mwingine wa leo, Alliance FC ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na African Lyon ya Dar es Salaam Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Lyon ilitangulia kwa bao la kiungo mshambuliaji, mkongwe Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya tisa kabla ya Mnigeria, Michael Chinedu kuisawazishia Alliance FC dakika ya 90 na ushei.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAENDELEZA UBABE LIGI KUU, YAICHAPA NDANDA FC 3-0 KUTINYU MAWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top