• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 22, 2018

  KAGERE AING’ARISHA SIMBA LIGI KUU, RUVU YAFA NYUMBANI…COASTAL YAAMBUA SARE MKWAKWANI…KAGERA SUGAR MOTO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameanza vyema Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Tanzania Prisons ya Mbeya bao 1-0 katika mchezo uliofanyika usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji kutoka Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere aliyefunga dakika ya pili kwa shuti kali baada ya kupewa pasi nzuri na Nahodha, John Raphael Bocco kutoka upande wa kulia.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hance Mabena kutoka Tanga, aliyesaidiwa Michael Mkongwa wa Njombe na Rashid Zongo wa Iringa, Simba ilitawala kipindi cha kwanza kwa kupeleka mashambulizi mengi kwenye eneo la Prisons, lakini uimara wa kipa Aaron Kalambo uliwanyima mabao zaidi.
  Mshambuliaji kutoka Rwanda, Meddie Kagera akishangilia baada ya kuifungia Simba SC bao pekee leo
  Meddie Kagere akimtoka beki wa Tanzania Prisons, Nurdin Chona
  Kiungo wa Simba SC, Hassan Dilunga akiwatoka wachezaji wa Prisons 
  Nahodha wa Simba SC, John Bocco akiruka juu kuwania mpira dhidi ya beki wa Tanzania Prisons, James Mwasote 

  Kipindi cha pili, Tanzania Prisons walibadilika na kuanza kupeleka mashambulizi ya nguvu langoni mwa Simba, lakini wakashindwa kutumia nafasi walizotengeneza.
  Katika mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Ndanda FC walipata ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Singida United wamefungwa 1-0 nyumbani Uwanja wa Namfua na Biashara United na Alliance FC pia imefungwa 1-0 na wapinzani wao wa jiji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Kagera Sugar imeanza vizuri kwa ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Coastal Union, timu kipenzi cha Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imelazimishwa sare ya 1-1 Lipuli FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Ligi hiyo itaendelea kesho, Yanga SC wakiwakaribidsha Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Saa 12:00 jioni, JKT Tanzania watamenyana na KMC kuanzia Saa 8:00 mchana Uwanja wa Meja Isamuhuyo, Stand United na African Lyon Saa 10:00 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na Azam FC na Mbeya City kuanzia Saa 2:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, James Kotei, Hassan Dillunga/Nicholas Gyan dk82, Meddie Kagere, John Bocco/Adam Salamba dk83 na Shiza Kichuya/Muzamil Yassin dk67.
  Tanzania Prisons; Aaron Kalambo, Benjamin Asukile, Laurian Mpalile, Nudrin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhili, Salum Kimenya, Cleophace Mkandala, Kelvin Friday/Lambert Sabiyanka dk82, Salum Bosco/Ramadhani Ibata dk71 na Ismail Aziz/Hassan Kapalata dk79.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGERE AING’ARISHA SIMBA LIGI KUU, RUVU YAFA NYUMBANI…COASTAL YAAMBUA SARE MKWAKWANI…KAGERA SUGAR MOTO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top