• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 28, 2018

  SAMATTA: NILIUGULIA MAUMIVU BAADA YA KUUPIGA MGUU WA AMPOMAH, LAKINI NIKO POA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameondoa hofu juu ya kuugulia maumivu Jumapili wakati wa mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena baina ya timu yake, KRC Genk na Waasland Beveren.
  Akizungumza kwa simu na Bin Zubeiry Sports - Online, Samatta aliyetokea benchi na kuifungia Genk ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Waasland Beveren juzi, amesema kwamba hakuumia, bali mguu ulishituka kidogo baada ya kugongana na kiungo Mghana, Nana Opoku Ampomah.
  “Nilipiga shuti lakini mguu wangu ukaenda kupiga kwenye mguu wa huyo mchezaji (Nana Opoku Ampomah), ila niliinuka kumalizia mchezo na ninaendelea vizuri tu,”alisema Samatta.

  Mbwana Samatta (chini) akiugulia maumivu baada ya kugongana na kiungo Mghana wa Waasland Beveren, Nana Opoku Ampomah (juu)

  Samatta aliingia uwanjani dakika ya 58 Jumapili usiku kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mbelgiji, Zinho Gano na ikamchukua dakika 20 tu kuifungia bao Genk akimalizia pasi ya kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy.
  Kabla ya kutoka, Gano alimsetia mshambuliaji Mkosovo mzaliwa wa Ujerumani, Edon Zhegrova kuifungia Genk bao la kwanza dakika ya 20 na bao lingine la timu hiyo limefungwa na mshambuliaji mwingine Mbelgiji, Leandro Trossard dakika ya 89.
  Mabao yote ya Waasland Beveren yamefungwa na Ampomah dakika za 66 na 75 na kwa matokeo hayo sasa Genk inapanda kileleni, ikifikisha pointi 13 baada ya mechi tano, ikiwa mbele ya Club Brugge yenye pointi 13 pia, Anderlecht pointi 12 na Standard Liege pointi 11 baada ya zote kucheza mechi tano tano pia.
  Genk watarudi uwanjani Alhamisi kumenyana na Brondby nchini Denmark katika mchezo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi ya Europa League wakitoka kushinda 5-2 kwenye mchezo wa kwanza, tena Samatta akifunga matatu peke yake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA: NILIUGULIA MAUMIVU BAADA YA KUUPIGA MGUU WA AMPOMAH, LAKINI NIKO POA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top