• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 23, 2018

  PLUIJM APANIA KUANZA LIGI NA USHINDI AZAM FC DHIDI YA MBEYA CITY LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans van der Pluijm, ameelezea mikakati yake kuelekea mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Mbeya City.
  Mholanzi huyo amesema kuwa jambo la muhimu ni kikosi chake kuanza vema msimu wa ligi kesho Alhamisi kwa kuibuka na ushindi dhidi ya timu hiyo yenye maskani yake jijini Mbeya, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 2.00 usiku.
  “Maandalizi yetu kuelekea ligi yamefanyika vizuri matarajio yetu ni makubwa nadhani sio kwetu tu ni kwa kila mtu hadi hivi sasa tuna majeruhi wawili ambao hawawezi kuwepo kwenye mechi ya kwanza watakaokuwepo kwenye mechi zinazofuata lakini nafikiri tuna timu nzuri.

  Hans van der Pluijm, amepania kuanza na ushindi mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City

  “Ninachojua kuhusu Mbeya City, siku zote wamekuwa wapinzani wagumu, sio tu wanapokutana na Azam FC au Simba au Yanga daima wamekuwa wakionyesha zaidi kuliko wanavyoonyesha mechi nyingine lakini najua kitu cha kufanya na ndio maana nipo hapa, tunatarajia mchezo mgumu,” alisema Pluijm.   
  Azam FC itaingia kwenye msimu mpya wa ligi ikiwa na morali kubwa baada ya kutwaa ubingwa wa pili mfululizo wa michuano ya Kombe la Kagame, ikiifunga Simba mabao 2-1, yaliyofungwa na mshambuliaji Shaaban Idd, aliyehamia CD Tenerife ya Hispania na nahodha Agrey Moris, aliyefunga la ushindi akizima bao lililosawazishwa na Meddie Kagere.
  Kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea, Ashanti Gold za Ghana, Singida United na Yanga, alisema ugumu wa mchezo huo sio kitu kwani kila mechi si sawa akidai anaamini wataibuka na ushindi baada ya dakika 90.
  “Cha muhimu ni timu yetu kucheza kwa mpangilio na kutofanya makosa na kutumia nafasi tunazopata na mwisho wa siku baada ya dakika 90 naamini tutaibuka na ushindi,” alisema.
  Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana ndani ya Azam Complex, Azam FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Mbaraka Yusuph.
  Akizungumzia mchanganyiko wa wachezaji wapya na wale wa zamani, alisema muunganiko ni mzuri na kwenye timu kuna hali nzuri huku pia kukiwa na mawasiliano mazuri.
  “Nafikiri kuna hali nzuri kwenye timu ambalo ni jambo muhimu, kuna mawasiliano katika timu wakati tukiwa kambini wanajuana vizuri (wachezaji), angalia baada ya dakika 90 tunaweza kusema mambo yameenda vizuri au la.
  “Unaweza kujiandaa vizuri sana na matokeo yakawa tofauti huo ndio mpira kawaida hautabiriki lakini tunaenda kwa ajili ya pointi tatu hilo ndio jambo la msingi kwetu kuanza ligi na matokeo mazuri sio kwetu tu bali kwa familia yote ya Azam, mashabiki na uongozi,” alisema.
  Wachezaji wapya waliosajiliwa na Azam FC ni mabeki Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, ikimrejesha kiungo wake Mudathir Yahya, washambuliaji Tafadzwa Kutinyu, Danny Lyanga, Ditram Nchimbi na Donald Ngoma.
  Lyanga amekuwa kwenye kiwango kizuri kwenye mechi za majaribio za msingi, ambapo katika mechi tatu alizocheza amefunga jumla ya mabao mawili huku mshambuliaji mwingine Nchimbi akifunga mabao mawili katika michuano iliyopita ya Kagame.
  Kihistoria Azam FC na Mbeya City zimekutana mara 10 kwenye ligi, tokea timu hiyo ya jijini Mbeya ilivyopanda daraja mwaka 2013, Azam FC ikiwa imeshinda asilimia 95 ya mechi zote ikiibuka kidedea mara tano, sare nne na kupoteza mara moja.
  Mchezo ilioupoteza ilitokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka pointi tatu Azam FC baada ya kushinda mabao 3-0 jijini Mbeya, ikidai ilimchezesha beki Erasto Nyoni kimakosa kutokana na mchezaji huyo kukusanya kadi tatu za njano.
  Azam FC imepania kufanya vizuri zaidi msimu huu kwa kutwaa ubingwa wa ligi, baada ya msimu uliopita kushika nafasi ya pili nyuma ya Simba, ili kudhihirisha hilo imefanya usajili mzuri pamoja na kuajiri makocha wenye uzoefu wa ligi Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi na Kocha wa Makipa aliyebakia, Idd Abubakar.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PLUIJM APANIA KUANZA LIGI NA USHINDI AZAM FC DHIDI YA MBEYA CITY LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top