• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 21, 2018

  SERENGETI BOYS YAENDELEZA UBABE MICHUANO YA CECAFA KUFUZU AFCON 2019, YAICHAPA RWANDA 4-0

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imefanikiwa kumaliza juu ya Kundi A michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA AFCON Qualifier) baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Rwanda jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Serengeti Boys inafikisha pointi tisa baada ya kucheza mechi tatu na kushinda zote, hivyo kumaliza kileleni mwa Kundi A, wakati Rwanda inamaliza nafasi ya pili na zote tayari zimefuzu Nusu Fainali, huku Burundi na Sudan zikiaga.

  Katika mchezo wa leo, mabao ya Tanzania yamefungwa na Kelvin John matatu dakika za 22, 82 na 90 na ushei wakati lingine limefungwa na Agiri Ngoda dakika ya 77.
  Sasa Serengeti Boys na Amavubi Junior wanasubiri matokeo ya mechi za kesho za Kundi B kati ya Uganda na Djibouti na Ethiopia na Kenya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ili kujua wapinzani wao wa Nusu Fainali.
  Ethiopia inaongoza Kundi B kwa pointi zake tisa za mechi tatu, ikifuatiwa na Uganda yenye pointi sita sawa na Kenya, wakati Sudan Kusini ina pointi tatu na Djibouti imemalizia mkiani ikiwa haina pointi.
  Tanzania ndiyo wenyeji wa Fainali za AFCON U17, michuano inayotarajiwa kuanza Mei 12 hadi 26 mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAENDELEZA UBABE MICHUANO YA CECAFA KUFUZU AFCON 2019, YAICHAPA RWANDA 4-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top