• HABARI MPYA

    Tuesday, August 21, 2018

    AMUNIKE AMTEMA 'BANKA' TAIFA STARS...AITA 25 KUIVAA UGANDA SEPTEMBA 8 KAMPALA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mnigeria Emmanuel Amunike hajamuita kiungo mpya wa Yanga, Mohammed Issa ‘Banka’ katika kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala.
    Banka alicheza vizuri Taifa Stars ikiifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) 2-0 katika mchezo wake wa mwisho Machi 27, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, ambao ulikuwa wa kirafiki.


    Mohammed Issa 'Banka' hajaitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mchezo na Uganda Septemba 8 mjini Kampala

    Lakini katika mkutano wake na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Amunike amewarejesha asilimia kubwa ya wachezaji waliokuwemo kwenye kikosi cha Stars mara ya mwisho, isipokuwa Banka aliyejiunga na Yanga SC kutoka Mtibwa Sugar.
    Hao pamoja na makipa watatu Aishi Manula wa Simba SC, Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, Benno Kakolanya wa Yanga SC.
    Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba SC), Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Gardiel Michael (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Kelvin Yondan (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam FC) na Andrew Vincent ‘Dante’ (Yanga SC).
    Viungo ni Himid Mao (Petrojet FC, Misri), Mudathir Yahya (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadida, Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (CD Tenerife, Hispania), Feisal Salum (Yanga SC) na Hassan Dilunga (Simba SC).
    Washambuliaji ni Rashid Mandawa (BDF XI, Botswana), Yahya Zayed (Azam FC), Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife, Hispania), John Bocco (Simba SC), Emmanuel Ulimwengu (El HIlal, Sudan) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).
    Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    Amunike amesema kwamba katika kukinoa kikosi hicho atasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi pamoja na Mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE AMTEMA 'BANKA' TAIFA STARS...AITA 25 KUIVAA UGANDA SEPTEMBA 8 KAMPALA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top