• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 26, 2018

  UGANDA WAFALME WA SOKA YA VIJANA CECAFA, WAUNGANA NA SERENGETI BOYS AFCON U17 DAR 2019

  Na Amina Ismail, DAR ES SALAAM
  UGANDA wameendelea kudhihirisha ubora wao katika soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa ukanda wa Afrika Mashariki (CECAFA AFCON Qualifier 2019) kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ethiopia leo Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
  Ushindi huo umetokana na mabao ya Kasozi Samson dakika ya 14 na Abdulwahid Iddi, mawili dakika za 61 na 85 wakati la Ethiopia limefungwa na Mintesnot Wakigira dakika ya 90 na ushei na sasa The Kobs wataiwakilisha CECAFA kwenye AFCON U17 Mei mwakani hapa hapa Dar es Salaam.
  Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad aliwakabidhi Kombe la ubingwa wa michuano hiyo mipya Uganda mbele ya mamia ya mashabiki waliojitokeza Uwanja wa Taifa.
  Mapema katika mchezo uliotangulia wa kusaka mshindi wa tatu, Tanzania walishinda kwa penalti 4-3 dhidi ya Rwanda baada ya sare ya 2-2.
  Tanzania wamefuzu moja kwa moja kushiriki AFCON U17 Mei mwakani kwa sababu wao ndio wenyeji wa michuano hiyo.
  Ethiopia imetoa Kipa Bora wa Mashindano Alazar Mako na mfungaji bora, Mintesnot Endrias Wakijira aliyefunga mabao nane, wakati Mchezaji Bora ni Kelvin Pius John wa Tanzania iliyotwaa pia tuzo ya Mchezo wa Kiungwana.
  Timu nyingine zilizoshiriki michuano hiyo iliyoanza Agosti 11, mwaka huu ni Burundi, Djibouti, Kenya, Somalia, Sudan Kusini na Sudan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UGANDA WAFALME WA SOKA YA VIJANA CECAFA, WAUNGANA NA SERENGETI BOYS AFCON U17 DAR 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top