• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 28, 2018

  YANGA SC WAENDA KUCHEZA KIGOMA BAADA YA MIAKA 19…WATAMENYANA NA SINGIDA UNITED SEPTEMBA 5 LAKE TANGANYIKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC na Singida United zinatarajiwa kumenyana katika mchezo maalum wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma Septemba 5, mwaka huu.
  Huo utakuwa mchezo wa kwanza kwa mabingwa hao wa kihistoria nchini, Yanga SC kucheza mjini Kigoma baada ya miaka 19, kwani mara ya mwisho walicheza mwaka 1999 dhidi ya Mbanga FC na FC Kongo za huko.
  Na ndio huko walipomuona kwa mara ya kwanza winga Said Maulid Kalikula ‘SMG’ akiichezea FC Kongo, lakini wakachelewa kumsajili hadi akasajiliwa kwanza na mahasimu wao wa jadi Simba SC baadaye mwaka huo na kuanza kucheza msimu wa 2000.
  Hata hivyo, ndoto za SMG kucheza Yanga zilitimia mwaka 2002 aliposajiliwa kwa kishindo na kudumu hadi mwaka 2008 alipohamia Onze Bravos ya Angola hadi mwaka 2012 aliporejea nyumbani kumalizia soka yake klabu ya Ashanti United.

  Yanga na Singida United zinatumia mwanya wa baadhi ya mechi za Ligi Kuu kusimama kwa muda kupisha maandalizi ya mchezo wa Kundi L baina ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Uganda Septemba 8 mjini Kampala kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
  Kikosi cha Yanga SC kimeondoka Alfajiri ya leo kwenda mjini Kigali nchini Rwanda kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sport, kufuatia kushinda mechi moja tu kati ya tano za awali, kufungwa tatu na sare moja.
  Mchezo wa kesho utakaoanza Saa 9:00 Alasiri Uwanja wa Nyamirambo, utachezeshwa na marefa kutoka Uganda, Mashood Ssali atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Mark Ssonko na Dick Okello.
  Mchezo wa kwanza baina ya Yanga na Rayon Sport, wote mabingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati timu hizo zilimaliza kwa sare ya 0-0 Mei 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Yanga SC inashika mkia katika kundi D, ikiwa na pointi nne tu, nyuma ya Rayon yenye pointi sita, wakati Gor Mahia na USM Alger kila moja ina pointi nane na zinamenyana kwenye mechi ya mwisho Jumatano pia mjini Algiers.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAENDA KUCHEZA KIGOMA BAADA YA MIAKA 19…WATAMENYANA NA SINGIDA UNITED SEPTEMBA 5 LAKE TANGANYIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top