• HABARI MPYA

  Tuesday, October 03, 2017

  KINDA MTANZANIA ANAYECHEZA BUNDESLIGA ATAKA KUITWA TAIFA STARS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO Mtanzania, Michael John Lema anayechezea timu ya SK Sturm Graz yenye maskani yake Graz, Styria, Austria inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo, maarufu kama Bundesliga amesema ana hamu ya kuitwa timu ya taifa, Taifa Stars. 
  Kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya na futaa.com, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 17, amesema kwamba ndoto yake kubwa ni siku moja kuchezea timu yake ya taifa, Taifa Stars ingawa kwa sasa anachezea timu ya vijana za Austria chini ya umri wa miaka 17.
  “Nitafurahi sana iwapo siku moja nitaitwa katika Timu ya Taifa ya Tanzania, kwani huko ndio nyumbani kwetu, wazazi wangu wapo huko, familia yangu na ndugu zangu wapo huko, ila shida ni kuwa tayari nimeshachukua uraia wa Austria, lakini ikiwezekana kuitwa Taifa Stars nitafurahi sana,”alisema katika mahojiano yake na futaa.com hivi karibuni. 
  Michael John Lema akiwatoka wachezaji wa timu pinzani katika moja ya mechi anazcheza Austria  

  GONGA HAPA KUONA PICHA ZAIDI


  Historia ya Michael Lema inaanza Miaka 17 iliyopita katika Mkoa wa Singida, maeneo ya Itigi ambako Mzee na Bibi John Lema waliweza kuleta Duniani Kiumbe ambacho kwa wakati huo pengine wasingeweza kujua kuwa wanamleta Mwanandinga Bora.
  “Nimezaliwa Itigi Singida, Mimi nipo huku lakini wazazi wangu wote wapo Singida, Shule ya Msingi nilisoma hapohapo Itigi hadi Darasa la Nne ambayo ilikuwa ni mwaka 2009, ambapo nilikwenda Austria ambapo nilifikia kwa Rafiki wa mama Yangu, ambaye ndiye naweza kusema ni mfadhili wangu” Anaanza kusema Michael John Lema.
  Michael anasema lengo kubwa la yeye kuchukuliwa kwenda Austria lilikuwa kwa ajili ya Masomo lakini kuna kipindi alipenda kwenda uwanjani kufanya mazoezi na huko ndipo kipaji chake kilipoonekana.
  “Nilikuja huku kwa lengo la Masomo, lakini nilipofikisha miaka 10 nikaanza kuupenda mpira ambapo nilimuomba mfadhili wangu anipeleke uwanjani kufanya mazoezi ambapo nilicheza na wakaniona kuwa naweza kucheza vizuri, nakumbuka kuna siku  tulicheza na Sturm Graz ambapo kocha wao akaniona na kuniomba nijiunge na timu ya Watoto” Anasema.
  Anasema baada ya kupigiwa simu mara ya kwanza alikataa lakini baada ya kama majuma mawili kocha wa timu hiyo alimpigia tena na hapo ndipo Akamuomba mlezi wake ampeleke Mji wa Graz ilipo academy ya Timu hiyo na kusaini Mkataba na Timu hiyo.
  Mchezaji huyo ambaye anavaa Jezi namba 38 katika Timu ya Sturm Graz alikuwapo katika kikosi cha akiba kwenye mchezo wa kufuzu kwa michuano ya Uropa Ligi dhidi ya Fenerbahçe ya Uturuki na kupoteza kwa mabao 2-1 mchezo uliopigwa Julai 27 Katika mji wa Graz Austria.
  “Natamani sana niingie uwanjani nikiwa na Timu ya wakubwa hata nicheze dakika 2 tu nionyeshe uwezo wangu, unajua baada ya miaka mitatu hadi minne nataka nionekane zaidi kimataifa na kucheza Ligi Kuu ya England na nina imani kubwa kuwa hapo nitafika tu,” anasema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KINDA MTANZANIA ANAYECHEZA BUNDESLIGA ATAKA KUITWA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top