• HABARI MPYA

  Friday, September 15, 2017

  YANGA HATARINI KUMKOSA KAMUSOKO MECHI NA MAJI MAJI KESHO

  Na Prince Akbar, SONGEA
  YANGA iko hatarini kumkosa kiungo wake tegemeo, Mzimbabwe Thabani Kamusoko katika mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Maji Maji mjini Songea.
  Hiyo inafuatia mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Zimbabwe kutonesha maumivu ya nyonga katika mazoezi ya juzi mjini Njombe na kushindwa kumalizia.
  Kamusoko jana pia hakufanya mazoezi baada ya timu kuwasili mjini Songea tayari kwa mchezo wa kesho Uwanja wa Maji Maji na sasa atatazamwa leo kama ataweza kuingia uwanjani.
  Thabani Kamusoko katikati ya wachezaji wa Lipuli ya Iringa katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu

  Kwa mujibu wa Daktari wa Yanga, Edward Bavu kuna asilimia chache mno kwa Kamusoko kucheza mechi dhidi ya Maji Maji na zaidi kocha Mzambia, George Lwandamina anaweza kumuacha apone vizuri ili arudi kikamilifu katika mchezo utakaofuatia dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Septemba 23.   
  Kamusoko aliondoka uwanjani mwanzoni tu mwa kipindi cha pili baada ya kuumia nyonga katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu wa Yanga dhidi ya wenyeji Njombe Mji Septemba 10 Uwanja wa Saba Saba mjini humo.
  Katika mchezo huo, mshambuliaji mpya kutoka Simba, Ibrahim Hajib alifunga bao pekee mwanzoni mwa kipindi cha kwanza, Yanga ikishinda 1-0. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA HATARINI KUMKOSA KAMUSOKO MECHI NA MAJI MAJI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top