• HABARI MPYA

  Friday, September 15, 2017

  SIMBA KUMKOSA NIYONZIMA MECHI NA MWADUI JUMAPILI

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KIUNGO Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima hatakuwepo kwenye kikosi cha Simba Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga kutokana na kuwa majeruhi.
  Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliiambia Bin Zubeiry Sports – Online jana kwamba Haruna aliumia mazoezini wiki hii na hataweza kucheza Jumapili.
  Pamoja na Haruna, Mayanja amesema beki wa kulia, Shomari Kapombe ataendelea kukosekana, wakati mshambuliaji Juma Luizio naye ameingia kwenye orodha ya majeruhi na hatakuwepo Jumapili.
  Haruna Niyonzima hatakuwepo kwenye mchezo dhidi ya Mwadui FC Jumapili

  “Ni hao wachezaji watatu tu tutawakosa Jumapili, lakini wengine wote wapo vizuri na maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mchezo huo,”alisema.
  Mayanja amesema anatarajia utakuwa mchezo mgumu, lakini wamejipanga vizuri kuweza kushinda ili kuimarisha mkakati wa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
  “Ligi ni ngumu kwa ujumla, tunatarajia mchezo mgumu, lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda mchezo huo na kurudi kileleni mwa Ligi Kuu,”alisema Mayanga.
  Simba SC iliuanza msimu huu wa Ligi Kuu vizuri, ikishinda mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting Agosti 26 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kabla ya kwenda kulazimishwa sare ya 0-0 na Azam FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Septemba 9.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA KUMKOSA NIYONZIMA MECHI NA MWADUI JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top