• HABARI MPYA

  Wednesday, September 06, 2017

  TFF YAMFUNGULIA BUSWITA, YAAMUA ACHEZE YANGA

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Sheria Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungulia kutoka kwenye kifungo cha mwaka mmoja, kiungo wa Yanga, Pius Buswita.
  Mchezaji huyo alikuwa na adhabu hiyo kutokana na kosa la kusaini mikataba na timu mbili za Simba na Yanga na hivyo kamati hiyo kuamua kumfungia.
  Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Elias Mwanjala aliwaambia wanahabari jana kuwa, hatua ya kumfungulia imekuja baada ya pande tatu zinazohusika katika sakata hilo yaani Simba, Yanga na mchezaji husika wamekubaliana ambapo sasa Wekundu hao wa Msimbazi watalipwa pesa zao.
  Pius Buswita ameruhusiwa kuendelea na kazi Yanga SC baada ya Simba kukubali yaishe

  Wakili Mwanjala alisema kilichofanywa na klabu hizo mbili ni busara tu ili kumpa nafasi mchezaji huyo na aweze kulinda kiwango chake kinyume cha hapo mchezaji huyo angeendelea kutumikia adhabu hiyo kwani walichokitaka Simba wao ni kulipwa tu pesa zao ili kuondoa malalamiko hayo.
  Alisema, mchezaji huyo ameahidi mbele ya Kamati kuwa atalipa pesa hizo ambazo ni shilingi milioni 10 pamoja na gharama zingine ikiwa ni pamoja na usafiri na malazi ambazo kwa pamoja zinafikia milioni 1 ndizo zilizotajwa na Simba kwenye barua yao waliyoiwasilisha TFF na ndicho kiasi ambacho Yanga na mchezaji wameahidi kulipa.
  Kamati imetoa onyo kali la kimaandishi kwa mchezaji huyo na ataruhusiwa kucheza tu iwapo Simba watathibitisha kulipwa pesa zao.
  Buswita ambaye ni mchezaji wa zamani wa Mbao ya Mwanza, alifungiwa na kamati hiyo baada ya kusajiliwa na Yanga huku pia akiwa amesaini mkataba na Simba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YAMFUNGULIA BUSWITA, YAAMUA ACHEZE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top