• HABARI MPYA

  Friday, September 15, 2017

  MBEYA CITY YATAKA KUMALIZA HASIRA ZAKE KWA NJOMBE MJI

  Na Gwamaka Mwankota, MBEYA
  TIMU ya Mbeya City inajivunia kutokuwa na majeruhi hata mmoja kuelekea kwenye mchezo wake wa Jumapili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
  Daktari wa Mbeya City, Isaac Apolinary amesema leo mjini Mbeya katika mazungumzo na Bin Zubeiry Sports – Online kwamba wachezaji wote wako vizuri na afya tele kuelekea mchezo dhidi ya Njombe Mji iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
  Daktari huyo bingwa alisema hayo baada ya mazoezi ya leo asubuhi kujiandaa na mchezo huo na akaseam mshambuliaji Frank Hamis ‘Ikobelo’ na beki Erick Kyaruzi ‘Mopa’ walioumia katika mchezo uliopita dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Sokoine mjini hapa, Mbeya City ikifungwa 1-0 sasa wote wapo fiti.
  “Kikosi chetu kipo vizuri na hatuna majeruhi hata mmoja kuelekea mchezo wetu wa Jumapili, timu imeendelea na mazoezi leo chini ya Kocha Msaidizi, Mohammed Kijuso, ambaye anashikilia usukani baada ya Kocha Mkuu (Mmalawi) Kinnah Phiri kuondoka rasmi hapo juzi,”amesema Dk Apolinary.
  Kwa upande wake, Kocha Kijuso amesema kwamba vijana wako tayari kwa mchezo ujao na wanataka kushinda ili kurejesha heshima.
  “Kwa kweli baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Ndanda, wachezaji wote hawakufurahi na wamekuwa wakijibidiisha mazoezini ili wawe vizuri na waweze kushinda mchezo ujao,”amesema Kijuso.
  Wakati Mbeya City ilianza Ligi Kuu kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea Agosti 26 kabla ya kufungwa na Ndanda Septemba 10, Njombe Mji imepoteza mechi zote mbili nyumbani Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, kwanza ilifungwa 2-0 na Prisons ya Mbeya na baadaye 1-0 na Yanga Septemba 10.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBEYA CITY YATAKA KUMALIZA HASIRA ZAKE KWA NJOMBE MJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top