• HABARI MPYA

  Wednesday, September 13, 2017

  BANDA ACHEZA DAKIKA 90, BAROKA YASHINDA 3-1 UGENINI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda jana ameisaidia klabu yake, Baroka FC kushinda ugenini mabao 3-1 dhidi ya wenyeji, Chippa United katika mchezo wa Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini Uwanja wa Nelson Mandela Bay mjini Port Elizabeth.
  Banda aliyejiunga na timu hiyo kutoka Simba SC ya nyumbani, Tanzania baada ya awali kuchezea Coastal Union ya Tanga, jana alicheza kwa dakika zote 90 Baroka wakivuna pointi za ugenini.   
  Mabao ya Baroka yalifungwa na James Okwuosa aliyejifunga dakika ya 41 na Gift Motupa aliyefunga mawili, dakika ya 63 na 89, wakati la wenyeji lilifungwa na Katlego Mashego kwa penalti dakika ya 57.
  Abdi Banda (kulia) jana ameisaidia Baroka FC kushinda 3-1 ugenini dhidi ya Chippa United katika Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini

  Huo ni mchezo wa tatu wa PSL kwa Baroka na Banda msimu huu na ni ushindi wa kwanza, baada ya awali kutoa sare mbili, kwanza 0-0 na Polokwane City ugenini Agosti 19 na baadaye 1-1 na Orlando Pirates nyumbani Agosti 22.
  Na Banda ndiye aliyeinusuru Baroka kulala nyumbani mbele ya timu ya kocha wa zamani wa Uganda, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 72 kwa kichwa akimalizia kona, kufuatia Thabo Qalinge kuanza kuifungia Pirates dakika ya 41. 
  Baroka sasa inashika nafasi ya 6 kwenye msimamo wa PSL inayoshirikisha timu 16 kwa pointi zake tano, nyuma ya Orlando Pirates, Cape Town City FC, Mamelodi Sundowns na SuperSport United zenye pointi sita kila moja katika na Maritzburg United wanaoongoza kwa pointi zao saba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BANDA ACHEZA DAKIKA 90, BAROKA YASHINDA 3-1 UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top