• HABARI MPYA

    Tuesday, November 24, 2015

    STARS YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA CHALLENGE

    Na Mwandishi Wetu, KIGALI
    TANZANIA Bara imejihakikishia kwenda Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Rwanda katika mchezo wa Kundi A jioni ya leo Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Ethiopia.
    Ushindi huo, unaifanya Tanzania Bara iongoze Kundi A kwa kufikisha pointi sita na mabao sita, huku ikiwa imefungwa bao moja na sasa itamaliza na wenyeji Ethiopia ikiwa ‘haina presha’.
    Kilimanjaro Stars leo ilipata bao lake la kwanza kupitia kwa kiungo wa Simba SC, Said Ndemla kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 22 baada ya Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ kuchezewa rafu na mchezaji mwenzake wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza.

    Said Ndemla wa kwanza kushoto walioinama ameifungia bao zuri Kili Stars leo

    Winga wa Yanga SC, Simon Msuva na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara – akaifungia Stars inayofundishwa Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ bao la pili dakika ya 78.
    Rwanda ilipata bao lake la kufutia machozi kupitia kwa Jacques Tuyisenge dakika ya 85. Sasa Amavubi iliyoifunga Ethiopia 1-0 katika mchezo wa kwanza, itamaliza na Somalia waliofungwa 4-0 na Kili Stars.      
    Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kevin Yondan, Salum Mbonde, Himid Mao/Jonas Mkude, Simon Msuva, Said Ndemla, John Bocco, Elias Maguri na Deus Kaseke.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top