• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 21, 2015

  KIZZA ‘DIEGO’ APANIA KUWEKA HISTORIA ADDIS 2015

  MSHAMBULIAJI wa Uganda, Hamisi Kizza ‘Diego’ amesema anataka kuweka historia katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka huu nchini Ethiopia.
  Kizza anayechezea Simba SC ya Tanzania Bara amesema kwamba anafurahi hivi sasa yuko kwenye kiwango kizuri, hivyo anaamini atafanya vizuri.
  “Nataka niweke historia ya kufunga mabao na kuisaidia timu yangu kubeba taji. Nafurahi nipo katika kikosi kizuri chenye wachezaji waliozoeana na wenye uwezo mkubwa wote,”amesema.
  Hamisi Kizza 'Diego' amepania makubwa Challenge 2015

  “Nina matumaini kabisa ya kufanya vizuri hapa na kuisaidia timu yangu kubeba Kombe,”amesema Kizza.
  CECAFA Challenge inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo nchini Ethiopia wenyeji wakifungua dimba na Rwanda mjini Addis Ababa.
  Mchezo huo wa Kundi A utatanguliwa na mechi nyingine ya Kundi B, kati ya Burundi na Zanzibar.
  Tanzania Bara watatupa kete yao ya kwanza kesho, watakapomenyana na Somalia katika mchezo wa Kundi A, wakati mabingwa watetezi, Kenya watasuguana na mabingwa wa kihistoria, Uganda baadaye. 
  Mechi za mzunguko wa kwanza wa makundi zitakamilishwa keshokutwa, Sudan Kusini wakimenyana na Djbouti kabla ya Sudan na Malawi kufuatia baadaye.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIZZA ‘DIEGO’ APANIA KUWEKA HISTORIA ADDIS 2015 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top