• HABARI MPYA

    Saturday, November 21, 2015

    SIMBA SC YAPANIA MAVUGO LAZIMA ATUE MSIMBAZI, AVEVA ASEMA MAJWEGA NAYE…

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imesema mpango wake wa kumsajili mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo (pichani kushoto) unakwamishwa na klabu ya Vital’O ambayo haitaki kutoa ushirikiano kwao.
    Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba wanafanya jitihada za kuwapata viongozi wa Vital’O wazungumzie suala la Mavugo, lakini hawapati ushirikiano.
    “Kuna watu wanasema Mavugo kamaliza Mkataba Vital’O, lakini habari kutoka Vital’O zinasema bado ana Mkataba hadi mwishoni mwa msimu. Sasa inatuchanganya kwa kweli,”amesema.
    Hata hivyo, Aveva amesema dhamira bado ni kumsajili Mavugo na wanaendelea na jitihada kuhakikisha wanafanikiwa.
    Amesema iwapo watamkosa Mavugo, basi watamgeukia Mrundi mwingine, Kelvin Ndayisenga ambaye yeye wazi hana Mkataba.
    Aidha, Aveva amethibitisha klabu yake kuwaacha Mganda Simon Sserunkuma na Msenegali, Abdoulaye Pape N’daw na kumrejesha Mkenya, Paul Kiongera.
    Kuhusu Mganda mwingine, Brian Majwega ambaye jana alianza mazoezi na Simba SC, Aveva amesema winga huyo ameomba kufanya mazoezi na timu hiyo wakati huu ambao ana mgogoro na klabu yake, Azam FC.
    Pamoja na hayo, Aveva amesema Kamati ya Usajili ya klabu yake, chini ya Mwenyekiti, Zacharia Hans Poppe imepewa jukumu la kusajili mabeki wawili wa kati.
    “Kwa ujumla ripoti ya benchi la Ufundi imependekeza kusajiliwa mabeki wawili wa kati, kiungo wa pembeni mmoja na washambuliaji wawili,”amesema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAPANIA MAVUGO LAZIMA ATUE MSIMBAZI, AVEVA ASEMA MAJWEGA NAYE… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top