• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 24, 2015

  YANGA SC WALALAMIKA; “WACHEZAJI WETU WANACHOSHWA, KILA SIKU WAO TU TIMU YA TAIFA, HAKUNA WENGINE?”

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga SC imesema kwamba wachezaji wake wanachoshwa kutokana na wakati wote kutumika wao tu katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kiasi kwamba wanahofia baadaye watashindwa kuisaidia klabu yao katika wakati muhimu.
  Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Juma Mwambusi ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana kwamba idadi kubwa ya wachezaji wao muda mrefu wamekuwa wakiitumikia Taifa Stars.
  Amesema ni wachezaji hao hao ambao kwa kipindi chote pia wamekuwa tegemeo la klabu yao, hivyo dhahiri watakuwa wanachoka kutokana na kukosa muda wa kupumzika.
  Kocha Juma Mwambusi (kushoto) katika mahojiano mafupi na BIN ZUBEIRY - SPORTS ONLINE jana Uwanja wa Boko Veterani

  Mwambusi alisema kwamba alitarajia katika kikosi cha Tanzania Bara cha Challenge, makocha wangetoa fursa kwa wachezaji wengine badala ya wale wale wa Yanga kila siku.
  Na amesema hiyo ingesaidia hata kwa wao makocha wa timu ya taifa kuandaa wachezaji wengine wa baadaye wa timu yao, kuliko kila siku kutegemea wale wale.
  Ametolea mfano baadhi ya nchi zilizopo kwenye michuano hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge zimemekwenda na wachezaji tofauti na wale ambao zimekuwa zikiwatumia mara kwa mara.
  “Hii maana yake unaandaa wachezaji wa baadaye kwa ajili ya timu, lakini kila siku wachezaji wale wale, kwanza unawachosha. Mimi nilidhani hii Challenge wangechukua wachezaji wengine,”amesema.
  Lakini Mwambusi amesema zaidi inaathiri programu ya mazoezi ya timu yao, kwani kutokana na kuwa na wachezaji wengi Challenge, kwa sasa mazoezi yao yanapambwa na vijana wa kikosi cha pili, Yanga B zaidi.
  Kocha Mwambusi akiwafundisha vijana wa Yanga B jana Uwanja wa Boko Veterani

  “Na pia nina wasiwasi tutakapowahitaji sisi watusaidie labda watakuwa wamechoka, kwa sababu tunataka kuwatumia watusaidie tutetee ubingwa wetu wa Ligi Kuu na pia tuwatumia katika Ligi ya Mabingwa (Afrika) sasa wakiwa wamechoka hawatatusaidia,”amesema.  
  Yanga SC inaendelea na mazoezi yake katika Uwanja wa Boko Veterani, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam wakati huu ambao Ligi Kuu imesimama tangu mwanzoni mwa mwezi kupisha michuano ya CECAFA Challenge inayomalizika Desemba 5. 
  Na Yanga SC mbali na kuwa na wachezaji kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars (Ally Mustafa, Juma Abdul, Kevin Yondan, Salum Telela, Simon Msuva, Deus Kaseke na Malimi Busungu)– wengine wapo Zanzibar (Mwinyi Mngwali, Nadir Haroub, Said Juma na Matheo Simon), Rwanda (Haruna Niyonzima) na Burundi (Amissi Tambwe).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WALALAMIKA; “WACHEZAJI WETU WANACHOSHWA, KILA SIKU WAO TU TIMU YA TAIFA, HAKUNA WENGINE?” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top