• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 16, 2015

  CANNAVARO: TUTAKINUKISHA ALGERIA, AMA ZAO AMA ZETU KESHO

  Na Mwandishi Wetu, ALGIERS
  NAHODHA wa Tanzania, ‘Taifa Stars’, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ amesema kwamba watapambana kiume kesho kuhakikisha wanashinda ugenini dhidi ya Algeria na kufuzu hatua ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya Kombe la Dunia mwaka 2018 Urusi.
  Taifa Stars ililazimishwa sare ya 2-2 na Algeria Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza Raundi ya Pili kufuzu Kombe la Dunia na kesho timu hizo zitarudiana mjini Algiers kuanzia Saa 3:00 usiku.
  Na baada ya matokeo hayo, Taifa Stars sasa itahitaji lazima kushinda ugenini Jumanne au kupata sare ya kuanzia 3-3 ili kuingia hatua ya mwisho ya mchujo, ambayo itakuwa ya makundi.
  Nahodha Cannavaro (kulia) akimpongeza Maguri baada ya kufunga bao la kwanza Jumamosi

  “Tuliongoza 2-0, dhidi ya Algeria. Ilikuwa jambo kubwa sana, tukadhani tumemaliza, kumbe tulisahau tunacheza dhidi ya timu bora Afrika, tukawapa mwanya, wakakomboa mabao,”amesema Cananavro.
  Hata hivyo, Nahodha huyo amesema kesho hawatarudia makosa na watacheza kwa kushambulia kama ilivyokua Dar es Salaam.
  “Tutashambulia na kujilinda kwa umakini mno, tunataka mabao ya mapema, tutaingia kushambulia sana kusaka mabao ya mapema. Na tutakuwa makini katika ulinzi,”amesema.
  Katika mchezo wa kwanza uliochezeshwa na refa Keita Mahamadou aliyesaidiwa na Diarra Bala na Niare Drissa Kamony wote wa Mali, mabao ya Stars yalifungwa na Elias Maguri na Mbwana Samatta, wakati ya Algeria yalifungwa na Slimani Islam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CANNAVARO: TUTAKINUKISHA ALGERIA, AMA ZAO AMA ZETU KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top