• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 29, 2015

  ETHIOPIA NA UHABESHI WAO, SISI NI TANZANIA NA USWAHILI WETU!

  ETHIOPIA jana wamepenya katika ‘tundu la sindano’ kwenda Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
  Wenyeji hao wa fainali za mwaka huu wamefuzu kama moja ya washindi watatu bora, baada ya kuambulia pointi nne katika Kundi A, nyuma ya Tanzania Bara iliyomaliza na pointi saba na Rwanda pointi sita.
  Ilibaki kidogo tu Ethiopia watolewe jana, kama si beki wa Tanzania Bara, Salim Mbonde kujifunga dakika za majeruhi kuwapatia sare ya 1-1 wenyeji, baada ya Simon Msuva kutangulia kuwafungia wageni.
  Wakati dakika zinayoyoma kuelekea filimbi ya mwisho Ethiopia wakiwa nyuma kwa bao 1-0 Uwanja wa Kimataifa wa Awassa, sura za Wahabeshi zilikuwa zinatia huruma.

  Kwanza, walifurika uwanjani hakuna hata ‘pa kutemea mate’ katika mchezo huo ambao ilikuwa lazima washinde au watoe sare ili kwenda Robo Fainali.
  Pili, waliendelea kuishangilia kwa nguvu timu yao hata ilipokuwa nyuma kwa bao 1-0 – lakini baada ya kuona zimeonyeshwa dakika nne za majeruhi, wakaonekana wamekata tamaa.
  Sura za majonzi zilikuwa zinaonyeshwa kwenye Televisheni, wengine machozi yakiwalenga wakiisikitikia timu yao.
  Hakuna aliyesikikia kuzomea, wala kutukana – wote walikuwa wenye majonzi na masikitiko kuashiria upendo wa hali ya juu kwa timu yao.
  Na ghafla Uwanja wa Awassa uliripuka kwa shangwe, hoi hoi, nderemo na vifijo baada ya Mbonde kujifunga kuwapatia Wahabeshi bao la kusawazisha.
  Sasa Tanzania Bara watakutana tena na Ethiopia Jumatatu katika Robo Fainali na hakika siku hiyo Kilimanjaro Stars watakuwa na kibarua kizito.
  Wakati natazama mchezo dakika zikiyoyoma, kila zilipopitishwa picha za mashabiki au wapenzi wa Ethiopia niliwaza mambo mengi sana.
  Kubwa niliwaza, kama Ethiopia ndiyo ingekuwa Tanzania inaelekea kutolewa kabla ya mechi za mtoano kwenye michuano ambayo ni wenyeji, huko majukwaani kungekuwa na utulivu wa aina hiyo?
  Aina gani ya matusi, kashfa na kejeli vingetumika kuwadhalilisha wachezaji! Hakika Wahabeshi wanatufundisha mapenzi ya timu ya taifa yanaambatana na subira na uvumilivu, kitu ambacho kwa Tanzania si hulka yetu.
  Watanzania wao wanataka ushindi tu ndiyo wanaipenda timu, lakini tofauti na hapo kwa matokeo mengine, wanakandia na kuponda kiasi cha kukatisha tamaa.
  Real Madrid ilipofungwa nyingi na Barcelona nyumbani, Mtanzania anasema; “Mipango yao (Real) ilifeli” – lakini Taifa Stars ilipofungwa nyingi na Algeria ugenini, jibu lilikuwa jepesi tu; “Hawajui (siyo hatujui) mpira”.
  Kwa sasa Bara, Kilimanjaro Stars inafanya vizuri katika Challenge ‘wakaanga sumu’ wapo kimya wanasubiri iteleze wawaangushie magunia ya kashfa wachezaji na makocha.
  Inakuwa kama huwa wanaiombea mabaya timu ifanye vibaya, ili wapate cha kusema.
  Mtanzania mmoja alitabiri mapema, Taifa Stars itatolewa na Algeria na akajiona mjuvi yalipotimia na akafurahi mno. 
  Kwanza huwezi kusifiwa kwa utabiri wa mbabe kumpiga mnyonge. Hiyo ni wazi ni ndiyo matarajio. Kwa hivyo hupaswi kutamba; “Nilisema” kwa sababu wengi tu walijua ila waliamua kuwapa moyo wachezaji wao wapambane na kubaki kutumia maneno ya busara’ “Itakuwa mechi ngumu (siyo tutafungwa)”.
  Jana Wahabeshi wamenikosha sana na nikajua kwamba, siyo tu wachezaji wetu bado wana mengi ya kujifunza, bali hata Watanzania tuna mengi ya kujifunza kwa raia wa nchi wengine juu ya soka.
  Nimejua kwamba, siyo tu uwezo wa wachezaji wetu ni mdogo katika soka ya kimataifa, bali hata mapenzi yetu Watanzania kwa timu yetu na taifa letu ni haba.
  Na nikajionea tofauti ya Ethiopia na Uhabeshi wao, na Tanzania na uswahili wetu. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ETHIOPIA NA UHABESHI WAO, SISI NI TANZANIA NA USWAHILI WETU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top