• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 30, 2015

  STARS YANG’OLEWA KWA MATUTA CHALLENGE, KAPOMBE NA JONAS MKUDE WAKOSA PENALTI

  Na Mwandishi Wetu, ADDIS ABABA
  TANZANIA Bara imetolewa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na wenyeji Ethiopia, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
  Katika mchezo huo wa Robo Fainali uliofanyika Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Tanzania Bara walikuwa wa kwanza kupata kupata bao liliofungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyemalizia krosi ya Deus Kaseke dakika ya 25.
  Ethiopia walisawazisha kwa penalti ya utata iliyofungwa na Nahodha wake, Panom Gathouch baada ya Mohammed Naser kujiangusha wakati akidhibitiwa na Shomary Kapombe dakika ya 57.
  Wachezaji wa Stars wakimpongeza Nahodha wao, John Bocco baada ya kufunga bao la kuongoza
  Nahodha wa Stars, John Bocco akiwa haamini macho yake baada ya kutolewa  Stars walionekana kutaka kupagawa baada ya wapinzani wao kusawazisha bao na kuanza kuwaletea ubabe marefa, lakini baadaye wakatulia na kuendelea kucheza mpira.
  Hata hivyo, bado bahati haikuwa yao, kwani baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1, walitolewa kwa matuta.
  Beki Shomary Kapombe na kiungo Jonas Mkude walikwenda kupoteza penalti zao, wakati waliofunga kwa upande wa Kilimanjaro Stars ni kiungo Himid Mao, mshambuliaji Bocco na beki Hassan Kessy.
  Waliofunga penalti za Ethiopia ni Panon Gathouch, Mohammed Naser, Ashalew Tamene na Behaylu Girima.  
  Katika Robo Fainali ya Kwanza, Uganda imeifunga 2-0 Malawi mabao ya Farouk Miya na Ceasar Okhuti na sasa itakutana na Ethiopia katika Nusu Fainali, wakati Kili Stars inarejea nyumbani Dar es Salaam.
  Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Said Mohamed, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kevin Yondan, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Simon Msuva, Himid Mao, John Bocco, Said Ndemla na Deus Kaseke.
  Ethiopia; Abel Mamo, Yared Bayeh, Aschalew Tamane, Anteneh Tesfaye, Aschalew Girma, Eliyas Mamo, Zekariyas Tuji, Gothuoch Panom, Beneyam Belay, Mohammed Naser na Bereket Yisshak.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: STARS YANG’OLEWA KWA MATUTA CHALLENGE, KAPOMBE NA JONAS MKUDE WAKOSA PENALTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top