• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 28, 2015

  KILI STARS KAZINI TENA LEO CHALLENGE, YAMENYANA NA WENYEJI ETHIOPIA

  Na Mwandishi Wetu, ADDIS ABABA
  HATUA ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inahitimishwa leo kwa michezo miwili.
  Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ itamenyana na wenyeji, Ethiopia ‘Walya’ mjini Awassa katika mchezo wa Kundi A na Uganda itapambana na Burundi katika mchezo wa Kundi B.
  Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ amesema kwamba leo watacheza kwa tahadhari ili kutunza nguvu zao kwa ajili ya Robo Fainali.
  Kibadeni amesema watapigania ushindi, lakini hawatatumia nguvu nyingi kukwepa kujichosha na wachezaji kuumia, wakati timu imekwishatinga Robo Fainali.
  Kikosi cha Kilimanjaro Stars kinachofanya vizuri Kombe la Challenge 2015 Ethiopia

  “Tunajua wenzetu wanataka sana ushindi ili waende Robo Fainali. Na kwa sababu ni wenyeji, tunatarajia hata marefa watakuwa upande wao. Tutajaribu kupambana tusipoteze mchezo. Hilo ndilo kubwa,”amesema Kibadeni.
  Kwa ujumla mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa nchini, amesema wachezaji wake wako vizuri kuelekea mchezo wa jioni ya leo na ana matumaini ya ushindi.
  Kili Stars imejihakikishia Robo Fainali baada ya ushindi mfululizo katika mechi mbili za awali, 4-0 dhidi ya Somalia na 2-1 dhidi ya Rwanda na leo inakamilisha mechi zake za Kundi A ikiwa kileleni. 
  Mechi nyingine za mwisho za makundi zilichezwa jana, Zanzibar ikiifunga Kenya mabao 3-1, wafungaji, Suleiman Kassim ‘Selembe’ mawili na Khamis Mcha ‘Vialli’ moja, wakati bao la Harambee Stars lilifungwa na Jacob Keli.
  Rwanda imeifunga 3-0 Somalia, mabao ya Jacques  Tuyisenge, Yussufu Habimana na Hegman Ngomirakiza, wakati Sudan Kusini iliifunga 2-0 Malawi, mabao ya James Joseph Saed na Bruno Martinez.
  Sudan iliifunga Djibouti 4-0, huku gwiji wake, Athar El Tahir akipiga hat-trick ya kwanza ya mashindano na bao lingine likifungwa na Faris Abdalla Mamoun.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KILI STARS KAZINI TENA LEO CHALLENGE, YAMENYANA NA WENYEJI ETHIOPIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top