• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 24, 2015

  KIPIMO MUHIMU KWA STARS LEO, YAMENYANA NA RWANDA

  ILIPOIFUNGA Somalia 4-0 katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi A Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baadhi ya ‘Watanzania’ walisema imeonea vibonde.
  Lakini leo timu ya taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars, inashuka tena Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Ethiopia katika mfululizo wa michuano hiyo, kumenyana na Rwanda ‘Amavubi’.
  Bila shaka Rwanda inaheshimika na hawawezi kuitwa vibonde – maana yake huo ni mtihani muhimu kwa kikosi hicho cha kocha mkongwe, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ anayesaidiwa Juma Ramadhani Mgunda.
  Kila la heri Kilimanjaro Stars leo dhidi ya Rwanda mjini Addis Ababa 

  Bara inahitaji ushindi tu katika mchezo huo utakaoanza Saa 11:00 jioni ili kujihakikishia kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo kama ilivyo ada yake.
  Na kocha Kibaden amesema anafahamu Rwanda ni timu nzuri baada ya kuiona awali ikiwafunga wenyeji, Ethiopia 1-0, lakini watajitahidi kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na Simba SC, amesema vijana wake wapo vizuri na jana wamefanya mazoezi mepesi kujiweka fiti kwa ajili ya Amavubi.
  “Tunatarajia utakuwa mchezo mgumu, lakini tutacheza kwa makini kutafuta matokeo na pia kutunza nguvu na utimamu wetu wa miili kwa ajili ya mchezo wa mwisho dhidi ya wenyeji, (Ethiopia) ambao ndiyo utakuwa mgumu zaidi,”amesema Kibaden. 
  Mchezo huo utatanguliwa na mchezo wa Kundi B, kati ya mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Uganda dhidi ya Zanzibar wenye rekodi ya kutwaa mara moja tu taji hilo, 1995 mjini Kampala.
  Na wote Zanzibar na Uganda walianza vibaya michuano hiyo, baada ya kufungwa katika mechi zao za kwanza, Heroes ikilala 1-0 mbele ya Burundi, wakati The Cranes ilitundikwa 2-0 na Kenya.
  Maana yake, kwao huo ni mchezo wa kupigania ushindi ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.  Leo kazi tu!
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIPIMO MUHIMU KWA STARS LEO, YAMENYANA NA RWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top