• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 28, 2015

  COUTINHO KUMPISHA ‘STRAIKA’ HATARI YANGA SC, HATIMA YAKE KUJADILIWA JUMATATU

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KIUNGO Mbrazil, Andrey Coutinho amerejea jana mjini Dar es Salaam na Jumatatu atakuwa na kikao na uongozi wa Yanga SC kujadili mustakabali wake katika klabu hiyo.
  Pamoja na kulipwa dola za Kimarekani 3,000 (zaidi ya Sh. Milioni 6) kwa mwezi, lakini Coutinho ameshindwa kumshawishi kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.
  Na kwa sababu hiyo, uongozi unaona hasara kuendelea na mchezaji anayelipwa fedha nyingi, wakati hachezi.
  “Hata kama ni mchezaji mzuri, kwa kuwa hana nafasi mbele ya Pluijm na sisi hatuna mpango wa kuachana na huyu kocha kabisa, hivyo haina maana kuendelea kuwa na Coutinho,”kimesema chanzo kutoka Yanga SC.
  Andrey Coutinho alikuwa anapata nafasi ya kucheza zaidi wakati wa Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo

  Kikao cha uongozi wa Yanga SC na Coutinho kinatarajiwa kujadili uwezekano wa mchezaji huyo kuvunjiwa Mkataba au kuhamishiwa timu nyingine moja ka moja.
  Na kumekuwa na taarifa kwamba klabu kadhaa ikiwemo za St George ya Ethiopia zinamtaka mchezaji huyo – hivyo Yanga SC iko tayari kumuacha kwa sasa.
  Na lengo la Yanga ni kutumia nafasi itakayoachwa wazi na Coutinho kwa kusajili mshambuliaji mwingine wa kigeni hatari zaidi ya iliyonao nao sasa ili kuimarisha kikosi chake kabla ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.   
  Coutinho alisajiliwa msimu uliopita Yanga SC chini ya kocha Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo na hadi sasa ameichezea klabu hiyo mechi 36 na kuifungia mabao saba.
  Alikuja nchini pamoja na mshambuliaji mwingine, Mbrazil Genilson Santana Santos ‘Jaja’ ambaye aliachwa baada ya nusu msimu akiwa amecheza mechi 11 na kufunga mabao matano.
  Wachezaji saba wa kigeni wanaokidhi kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania katika kikosi cha Yanga SC kwa sasa ni mabeki Mbuyu Twite (DRC), Vincent Bossou (Togo), viungo Haruna Niyonzima (Rwanda), Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Coutinho (Brazil) na washambuliaji Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: COUTINHO KUMPISHA ‘STRAIKA’ HATARI YANGA SC, HATIMA YAKE KUJADILIWA JUMATATU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top