• HABARI MPYA

    Sunday, November 15, 2015

    WASIOSTAHILI WALIFUKUZWA SIMBA SC, WANAOSTAHILI…

    MAMBO yanazidi kwenda ovyo katika klabu kongwe nchini, Simba SC kufuatia kocha Msaidizi, Suleiman Abdallah Matola kujiuzulu katikati ya wiki na kuweka wazi sababu ni tofauti zake na bosi wake, Muingereza, Dylan Kerr.
    Nahodha huyo wa zamani wa Simba SC, Matola amesema kwamba amefikia uamuzi huo baada ya kuona maelewano na bosi wake huyo yanazidi kuwa magumu kila kukicha.
    “Ni jambo la muda mrefu, huyu kocha hasikilizi ushauri wangu, imefikia sasa ananichukia na kazi haziendi tena. Sasa nimeona ili kuepusha matatizo zaidi, nimuachie yeye timu,”amesema Matola.
    Matola amesema kwamba haoni mwelekeo wowote mzuri kwa Simba SC chini ya kocha huyu Muingereza ambaye hasikilizi ushauri, ndiyo maana ameamua kujitoa.

    “Nimekutana na uongozi, nimewaambia juu ya uamuzi wangu, wakanisihi sana nisifanye hivyo, lakini nikashikilia msimamo wangu. Wakaniambia hata nirudi kufanya kazi timu za vijana, lakini nikawaambia nitajifikiria kwanza,”amesema Matola. 
    Historia ya Matola ndani ya Simba SC inaanzia mwaka 2000 alipojiunga nayo kama mchezaji akitokea Kagera Stars (sasa Kagera Sugar) na aliichezea timu hiyo hadi mwaka 2005 alipohamia Super Sport United ya Afrika Kusini.
    Matola alirejea Simba SC mwaka 2007 na kucheza kwa msimu mmoja kabla ya kustaafu moja kwa moja.
    Kuanzia mwaka 2010 amekuwa kocha wa timu za vijana za Simba SC ambako baada ya kufanya vizuri akapandishwa kuwa Kocha Msaidizi, akianza kufanya kazi na Mcroatia Zdravko Logarusic, baadaye Mzambia, Patrick Phiri, Mserbia, Goran Koponovic na huyu wa sasa Kerr.
    Haijawahi kutokea Matola akatofautiana na kocha yeyote kati aliyofanya nao kazi awali – na Muingereza huyu anakuwa wa kwanza kutofautiana na Nahodha wa zamani wa Simba SC.      
    Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva siku iliyofuata alinukuliwa akibariki kujiuzulu kwa Matola na kumtakia ‘kila la heri’ huko aendako.
    Pamoja na hayo, haitoshi tu kubariki kuondoka kwa Matola – bali uongozi wa Simba SC una kazi zaidi ya kufanya ili kuhakikisha hali inakuwa shwari katika timu.
    Simba SC inaweza kuajiri kocha Msaidizi mwingine, hata wa kigeni, lakini iwapo haitafanyia kazi tuhuma za Matola, tena kwa kina, matatizo yataendelea.
    Viongozi wa Simba SC ni mashahidi, kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Mserbia Dusan Momcilovic aliondoka miezi miwili iliyopita akiwa haelewani na Kerr.   
    Na viongozi mmoja mmoja wa Simba SC ‘kwa siri’ wamekuwa wakimponda kocha wao Kerr kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ufundishaji wake na mbinu zake kwa ujumla.
    Lakini ukiwauliza kwa nini wanahofia kuchukua hatua? Eti wamefukuza makocha wengi ndani ya muda mfupi, wanahofia wakimuondoa na huyo hawataeleweka.
    Maana yake, wako radhi labda timu iendelee kutitia kwenye tope la matatizo, tu kwa kuhofia kumuondoa mtu ambaye wamejiridhisha hafai kwa sababu waliwaondoa kimakosa walimu waliotangulia.
    Hii si sahihi – viongozi wa Simba SC wanapaswa kuendelea kuchukua hatua hadi hapo timu itakaposimama imara.
    Wengi walianza kumtilia shaka Kerr pale alipoagiza mshambuliaji Elias Maguli aachwe eti kwa sababu anakosa mabao mengi.
    Alimuacha Maguri wakati alikuwa anafunga mabao karibu kila mechi ya kirafiki aliyompanga. Na viongozi wa Simba SC wakaafikiana naye. 
    Sasa leo Maguri anaendelea kung’ara akiwa timu nyingine, Stand United kiasi cha kurejeshwa timu ya taifa, Taifa Stars na jana akaanza na kufunga bao katika mechi dhidi ya Algeria.
    Lakini hata upangaji wake wa timu kocha huyo ni haueleweki wakati mwingine amekuwa akiiponza dhahiri timu kupoteza mchezo kwa upangaji mbovu wa timu, mfano mechi dhidi ya Prisons mjini Mbeya.
    Kweli kuna wakati Simbs SC walifukuza makocha bila sababu za msingi, lakini huyu wa sasa unaona kabisa wana sababu za kuachana naye.
    Na si kwa sababu ya Matola, bali utendaji wake na maamuzi mabovu kwa ujumla ambayo dhahiri yanaigharimu timu kwa sasa.
    Wakati anamuacha Maguri, alisema ana washambuliaji wengine wengi chipukizi ambao ni wazuri kuliko mshambuliaji huyo. Sasa mbona hatuwaoni?
    Alikwishaanza ‘kumpoteza’ mshambuliaji mwingine hodari chipukizi, Ibrahim Hajib kwa kumuweka benchi, kabla ya kupigiwa kelele na uongozi, ndipo akamrejesha na faida yake akaiona, kwani amemfungia mabao muhimu.
    Kocha wa aina hii huwezi kuwa na imani naye na huwezi kuwa na sababu ya kuendelea naye- labda tu uwe umechoka kifikra na uamue kufanya mambo yaende kadiri itakavyowezekana. Kwa leo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WASIOSTAHILI WALIFUKUZWA SIMBA SC, WANAOSTAHILI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top