• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 22, 2015

  LABDA MUNGU ATASIKIA KILIO CHETU SIKU MOJA!

  KWA mara nyingine, Watanzania wamefedheheshwa na soka yao, baada ya timu yao ya taifa, Taifa Stars kutolewa na Algeria katika mbio za Kombe la Dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Urusi, baada ya kufungwa mabao 7-0 Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida Jumanne.
  Taifa Stars imetolewa kwa jumla ya mabao 9-2, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 na Mbweha hao wa Jangwani katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jumamosi wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
  Siku hiyo, Tanzania ilicheza pungufu kwa dakika 50 na zaidi, kufuatia kiungo Mudathir Yahya kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 40 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumkwatua Yacine Brahimi. Alitoka wakati Stars iko nyuma 2-0 na wenyeji wakatumia dakika 50 kupata mabao matano zaidi.

  Hakika kipigo hicho kimewaumiza Watanzania na wengi wanaonekana tena kukatishwa tamaa na soka yetu, jambo ambalo hakika ni baya.
  Wamesahau hata Taifa Stars ingeweza kupata ushindi mnono katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam kama wachezaji wangetumia vizuri nafasi walizopata na pia wasingefanya makosa yaliyoruhusu mabao ya wageni nyumbani.
  Watanzania wengi waliuona mchezo huo kupitia Televisheni, ukiachilia mbali wale zaidi ya Milioni 40 waliokuwa uwanjani na watakubaliana nami kwamba Stars ilipoteza nafasi tano za wazi za kufunga.
  Hapo sasa ndipo inapobidi kwanza tukubaliane na usemi “Soka ni mchezo wa makosa” – Waalgeria walifanya makosa Dar es Salaam, tukashindwa kutumia nafasi, lakini kwao hawakufanya makosa walipopata nafasi kutokana na makosa yetu.
  Walifunga mabao mawili kwa penalti na mawili kwa mipira ya adhabu nje kidogo ya boksi dhidi ya wapinzani pungufu uwanjani.
  Makosa yameigharimu Taifa Stars ndani na nje ya Uwanja na kutolewa na Algeria kwa aibu ya kipigo kikubwa ni malipo ya makosa hayo.
  Makosa ya kiufundi yalifanyika na yalionekana na hata benchi la Ufundi limekiri, lakini makosa zaidi yalifanyika nje ya Uwanja.
  Baada ya sare ya 2-2 na wenyeji Dar es Salaam, wachezaji wa Algeria walielekea kwenye hoteli ya Hyatt Regency (Kilimanjaro Kempinsky) kwa ajili ya mapumziko mafupi.
  Baada ya mapumziko yao ya takriban saa mbili, walioga na kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam ambako ndege yao waliyokuja nayo ilikuwa inawasubiri wao tu.
  Wakapanda ndege hiyo na kwenda moja kwa moja nyumbani, Algiers ambako walifika siku hiyo baada ya saa sita za angani.
  Na baada ya kufika Algiers, siku ilifyofuata wakaanza mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao wakati huo huo, wachezaji watatu ambao hawakuwepo katika mchezo wa kwanza wakaitwa kutoka Ulaya kuja kuongeza nguvu.
  Hao ni Mwanasoka Bora Afrika wa BBC mwaka jana, Yacine Brahimi, Belkaroui Hichem na Boudebouz Ryad, ambao wote walifika Jumapili jioni na Jumatatu walifanya mazoezi na wenzao.
  Taifa Stars, mara tu baada ya mchezo wa kwanza walikuwa wana kikao kifupi na Makamu wa Rais Dk. Samia Hassan Suluhu pale Uwanja wa Taifa.
  Baada ya hapo, wakarejea kambini kwao, hoteli ya Serena ambako baadaye tena wakawa na kikao na Kamati ya Taifa Stars, iliyowaahidi Sh. Milioni 500 iwapo wangeitoa Algeria.
  Kamati ya Taifa Stars iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Mecky Sadick waliwaweka mezani wachezaji kwa zaidi ya saa moja na nusu wakifanya nao mazungumzo baada ya chakula cha usiku.
  Kutoka hapo, wachezaji wakaenda kulala kwa saa mbili tu kabla ya kuamshwa kwa safari ya JNIA kusubiri ndege ya shirika la Uturuki, waende Algiers kupitia Istanbul.
  Wachezaji walikaa JNIA kwa saa mbili wakisubiri kuingia kwenye ndege ya Uturuki na kusafiri kwa saa nane kasoro kidogo hadi Istanbul, ambako walikaa kwa saa mbili kabla ya kuunganisha ndege kwenda Algiers ambako walitumia saa tatu.
  Msafara wa Taifa Stars ulifika Algiers saa 12 jioni za huko sawa na saa mbili usiku kwa saa za nyumbani- yaani baada ya kucha na kutwa za safari.
  Kutoka hapo, wakasafiri kwa basi kwa zaidi ya saa moja kwenda mjini Blida ambako baada ya kufika hawakupata muda wa mazoezi siku hiyo yote ya Jumapili.
  Siku iliyofuata ya Jumatatu, kutokana na uchovu wa safari, wachezaji walishinda hotelini tu kabla ya kwenda kufanya mazoezi kidogo tu kwa saa moja usiku wake Uwanja wa Mustapha Tchaker.
  Jumanne asubuhi makocha Charles Boniface Mkwasa na Msaidizi wake, Hemed Morocco waliongozana na wachezaji wao kufanya matembezi ya nusu saa kwenye mitaa ya jirani na hoteli yao mjini Blida.
  Baada ya hapo, wakarudi kupata kifungua kinywa, baadaye chakula cha mchana, kisha cha jioni pamoja na kupumzika kabla ya kwenda uwanjani kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
  Ni mchezo wa ugenini ambao Taifa Stars ilihitaji ushindi ili kuingia hatua ya mwisho ya mchujo wa Kombe la Dunia dhidi ya Algeria ambayo inatuacha mbali kwa kila kitu kiuwezo na uwekezaji kwenye soka.
  Baada ya dakika 45 tu, tayari Stars ilikuwa imekwishapigwa mabao matatu na kipindi cha pili wakaongezwa manne na kulala kwa 7-0, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 9-2.
  Ni kweli Algeria wanatuzidi uwezo, tena sana, lakini bado matumaini ya kupata matokeo mazuri ugenini yalikuwapo, iwapo wachezaji wasingechoshwa baada ya mchezo wa kwanza.
  Ukifuatilia ratiba ya Stars baada ya mchezo wa kwanza Dar es Salaam ukalinganisha na ya Algeria baada ya mchezo huo – kuelekea mchezo wa marudiano, huwezi kustaajabu sana timu yetu ilicheza kichovu na kufungwa mabao mengi.
  Kabla ya kuanza kufikiria sababu nyingine zote, kuhujumiwa au fitina za wenyeji, ukirudi kwenye ratiba ya timu baada ya mchezo wa kwanza kuelekea mchezo mwingine, unagundua mchawi wa kwanza ni wahusika wa timu. 
  Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wale wa Kamati ya Taifa Stars kwa kuipitisha timu safari ndefu kwenda Algiers kupitia Uturuki na vikao vingi vilivyowanyima wachezaji japo muda wa kuutathmini mchezo wa kwanza.
  Ni wazi wachezaji wa Taifa Stars walifika Algiers wakiwa wamechoka mwili na akili na hawakuwa tayari kuhimili mchezo mwingine mgumu kuliko ule wa Dar es Salaam.
  Haya ni mambo ambayo wakati tunajadili marefa na fitina za wenyeji, lazima yajadiliwe pia ikiwa tunataka kufanya vizuri katika mashindano mengine.
  Algeria wanaongeza silaha za vita, sisi tunazichosha silaha zetu kuelekea vitani.
  Kama Waalgeria walitufanyia figisu kuelekea mchezo wa marudiano, basi hazikuwa na madhara makubwa kuliko fitina tulizojifanyia wenyewe.
  Mpango wa awali ulikuwa Taifa Stars isafiri kwa ndege ya kukodi ya Fats Jet kwenda Algiers, ikawaje tena timu ikatumia ndege ya Uturuki?
  Ndege ya kukodi siyo tu ingepunguza muda wa safari angani – bali pia ingetufanya tujipangie wenyewe ratiba yetu ya kuondoka.
  Kuwanyima wachezaji muda wa kupumzika na kuutathmini mchezo wa awali, ilikuwa ni fitina nyingine mbaya ambayo tulijifanyia wenyewe pale Dar es Salaam.
  Yamekwishatokea na Wahenga walisema; “Maji yakimwagika hayazoleki”, kinachiotakiwa kwa sasa ni kuangalia mbele.
  Wachezaji wa Taifa Stars wamegawanywa kwenye vikosi vya Zanzibar na Tanzania Bara kwenda kwenye michuano ya CECAFA Challenge mjini Addis Ababa, Ethiopia iliyoanza jana hadi Desemba 5, mwaka huu.
  Baada ya hapo watarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Machi 25 watacheza na Chad mechi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017.
  Ikumbukwe Taifa Stars imekwishacheza mechi mbili bila kushinda, ilifungwa 3-0 na Misri ugenini na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria nyumbani – maana yake inahitaji kushinda mechi nne zilizobaki zikiwemo mbili za ugenini dhidi ya Chad na Nigeria ili kuangalia uwezekano wa kufuzu AFCON.
  Iwapo tutaendelea kuugulia maumivu ya kipigo cha Algeria na kusahau kujipanga kwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Chad Machi 25 ugenini na Machi 28 nyumbani, kabla ya kumaliza na Misri Juni 4 Dar es Salaam na baadaye Nigeria Septemba 2 Lagos, basi tutarajie maumivu mengine.
  Kila mmoja awajibike katika nafasi yake, Waandishi wa Habari tuandike kwa ajili ya kujenga na si kubomoa. Mashabiki wawe na subira. Viongozi (TFF) na wengine wasirudie makosa. Benchi la Ufundi lilerekebishe makosa.
  Tuliimba nchi nzima Taifa letu, timu yetu – basi tuendelee na moyo huo huo labda Mungu atasikia kilio chetu siku moja na ataibariki Tanzania katika medani ya soka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: LABDA MUNGU ATASIKIA KILIO CHETU SIKU MOJA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top