• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 25, 2015

  KWA NINI SIMBA SC KILA KUKICHA ‘MADUDU’ YALE YALE?

  WIKI hii baadhi ya magazeti yaliibuka na habari za wachezaji wa Cameroon kuja Simba SC kufanya majaribio.
  Na kama wakifuzu watasajiliwa kabla ya dirisha dogo kufungwa Desemba 15, mwaka huu ili waichezee timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Na Mpango huu ulikuja siku chache tu baada ya klabu hiyo kuamua kuachana na wachezaji wawili wa kigeni, winga Mganda Simon Sserunkuma na mshambuliaji Msenegali, Abdoulaye Pape N’daw.
  Wawili hao wameachwa kwa sababu wameshindwa kudhihirisha uwezo wao na hakuna lawama juu ya maamuzi yaliyochukuliwa.

  Sana lawama ni namna ambavyo walivyosajiliwa- Sserunkuma aliyekuwa katika msimu wake wa pili, alisajiliwa baada ya kung’ara katika mchezo wa kirafiki, akiichezea timu yake ya zamani, Express ya Uganda dhidi ya Simba, wakati N’daw alikuja majaribio Agiosti.
  Ukweli ni kwamba katika miaka ya karibuni, Simba SC wamekuwa wakifanya usajili wa kukurupuka mno na ule umakini uliokuwa sifa kuu ya klabu hiyo katika usajili miaka ya nyuma haupo tena.
  Watu bado wanakumbuka hadithi za akina Paschal Ochieng, Samuel Akuffo, Komalmbil Keita na hata Gilbert Kaze kama kielelezo cha usajili wa kukurupuka.
  Na hapo ndipo wanajiuliza hivi kweli hii ndiyo Simba iliyoibua vipaji vya wachezaji kama Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’, Nico Njohole, Abdul Ramadhani ‘Mashine’, Said Maulid ‘SMG’, Boniface Pawasa, Ramadhani Singano ‘Messi’ na wengine?
  Kinachosikitisha zaidi, Simba SC bado hawataki kujifunza kutokana na makosa na katika dirisha hili dogo wanataka tena kufanya usajili wa kukurupuka, wakati ni juzi tu Agosti iliingia mkenge kwa akina N’daw!
  Simba SC wanatakiwa kuelewa kwamba, mchezaji mzuri anatafutwa baada ya kutambulishwa na uwezo wake – ikiwa kuibua vipaji waende timu B.
  Simba A kwa sasa inahitaji kusajili wachezaji ambao tayari wamekwishadhihirisha uwezo wao katika Ligi nyingine au timu nyingine za hapa nchini.
  Na wachezaji wa aina hiyo wanapatikana kwa fedha na si maneno matupu. Na iwapo Simba SC hawajifunza kwa makosa waliyofanya miaka hii ya nyuma, basi wataendelea kuwa nyuma ya Azam na Yanga. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KWA NINI SIMBA SC KILA KUKICHA ‘MADUDU’ YALE YALE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top