• HABARI MPYA

    Thursday, October 01, 2015

    TAIFA STARS YA BAADAYE YAENDELEZA DOZI, YAWATANDIKA ‘MAFUNDI’ WA TANGA 4-0

    Na Mwandishi Wetu, TANGA
    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15, U-15 leo imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kujipima nguvu, baada ya kuichapa mabao 4-0 kombaini ya U-15 ya Tanga, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Ushindi huo umetokana na mabao mawili ya Issa Abdi dakika ya 21 na 23, Frank George dakika ya tisa na Ibrahim Abdallah Ali dakika ya 80.
    Pamoja na ushindi huo, lakini vijana wa U-15 ya Taifa, walikutana na ushindani kutoka kwa wachezaji wenye vipaji wa U-15 ya Tanga.
    Kivutio zaidi alikuwa ni kiungo Joseph Yakobo ambaye Tanga wanamuita ‘Sure Boy’ na mshambuliaji George Chande aliyeisumbua mno ngome ya timu ya taifa iliyoongozwa na Nahodha, Maulid Lembe.
    Wachezaji wa U-15 wakishangilia moja ya mabao leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga 

    Wachezaji wote waliokwenda majaribio Orlando Pirates ya Afrika Kusini mwezi uliopita, Asad Ali Juma, Issa Abdi Makamba, Kevin Deogratius Kahego, Amani Amede Maziku na Athumani Maulid Rajab walicheza leo.    
    Huo unakuwa mchezo wa tano kushinda, kati ya mechi saba tangu kuundwa kwa timu hiyo Aprili mwaka huu, ikifunga jumla ya mabao 15 na kufungwa mawili tu.
    Timu hiyo iliifunga 4-1 na 3-0 Mbeya, ikaifunga 4-0 na 1-0 Zanzibar na kutoa sare ya 0-0 na 1-1 na Morogoro kabla ya ushindi wa leo.
    Timu hiyo inayoandaliwa kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za vijana Afrika mwaka 2017 nchini Madagascar zitakazoanza Juni mwakani, imekuwa ikiweka kambi kila mwishoni mwa mwezi kwa ajili ya michezo ya kujipima nguvu, chini ya kocha wake, Bakari Shime.
    Kiungo wa U-15 ya taifa, Asad Ali juma akiwatoka wachezaji wa U-15 ya Tanga 


    Asad Ali Juma (kulia) akitafuta maarifa ya kumpokonya mpira mchezaji wa U-15 ya Tanga
    Mshambuliaji wa U-15 ya Taifa, Amani Maziku akimiliki mpira mbele ya wachezaji wa U-15 ya Tanga
    Beki wa kushoto wa U-15 ya Taifa, Faraj John (kulia) akimtoka mchezaji wa Tanga
    Kikosi cha U-15 ya Taifa kilichoifunga 4-0 Tanga leo 
    Kikosi cha U-15 ya Tanga kilichomenyana na U-15 ya taifa leo 


    Kesho, ‘Taifa Stars’ hiyo ya baadaye inatarajiwa kucheza mchezo wake wa mwisho mjini hapa, itakapomenana na U-17 ya mkoa Tanga hapa hapa, Mkwakwani.
    Wachezaji wote wa timu hiyo ni wanafunzi wa sekondari  mbalimbali nchini na ndiyo maana hukutanishwa mwishoni mwa mwezi tu kwa mazoezi ya pamoja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YA BAADAYE YAENDELEZA DOZI, YAWATANDIKA ‘MAFUNDI’ WA TANGA 4-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top