• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 18, 2015

  MALALAMIKO HAYA YA SIMBA SC NI YA KUFANYIWA KAZI, HAWATENDEWI HAKI

  KLABU kongwe ya Simba SC, inaonyesha haina imani na uongozi wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), chini ya Rais wake, Jamal Emil Malinzi.
  Hiyo inafuatia malalamiko yao ya mara kwa mara wakidai hawatendewi haki na shirikisho hilo na imani yao ni kwamba inasababishwa na uongozi wa TFF kusheheni watu wa Yanga SC.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amekaririwa wiki hii akisema kwamba, imefikia TFF wamekata kabisa mawasiliano na klabu yao.
  Poppe amesema kwamba TFF sasa hawajibu hata barua za Simba SC wanapoandika kuhoji au kuomba ufafanuzi wa jambo lolote.

  Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba imefikia wakati wanashindwa hata kujua namna gani wanaweza kupata haki zao nyingine za msingi, kutokana na ‘kuchuniwa’ na TFF.
  “Inafahamika kwamba Rais wa TFF (Jamal Malinzi), Katibu wake (Mwesigwa Selestine) wote ni Makatibu wa zamani wa mahasimu wetu, Yanga SC. Na bado wapo wengine wengi pale TFF ambao wametoka Yanga akina Baraka Kizuguto.
  “Lakini kwa sababu wanaongoza chombo cha kitaifa, wanapaswa kutenda haki, yaani inaonekana kabisa TFF wanaikandamiza Simba na wanaibeba Yanga,”amelalamika Poppe.
  Akifafanua, mfanyabiashara huyo maarufu nchini, amesema TFF hawajajibu barua yoyote ya Simba SC kwa mwaka huu na hawaelewei sababu ni nini.
  “Watuonyeshe wao, ni barua ipi ya Simba SC wamejibu mwaka huu, malalamiko yetu ya mchezo dhidi Yanga hawakujibu, Suala la Messi (Ramadhani Singano) hawakujibu. Hata tunapojibu barua zao za adhabu wanazotuandika ili kuomba ufafanuzi, pia hawatujibu. 
  “Labda watuambie basi kwamba barua zetu tunatakiwa kuzipitishia Yanga SC ndiyo watujibu, tutafanya hivyo, tutaandika na kuwapelekea Yanga waweke muhuri wao ipelekwe TFF, tujibiwe, hiyo ndiyo shida yetu,”amesema.
  Hans Poppe amesema kwamba mchezaji wao Ramadhani Singano ‘Messi’ amehamishiwa Azam FC kinyume cha utaratibu na kila wapodai haki yao hawasikilizwi. 
  “Mchezaji wa Yanga (Donald Ngoma) alimpiga kichwa mchezaji wetu (Hassan Kessy) na tukapeleka ushahidi wa picha za video, hakuchukuliwa hatua na wala hatukujibiwa,”. 
  “Lakini Juma Nyosso (wa Mbeya City) alimdhalilisha John Bocco (wa Azam FC) akachukuliwa hatua baada ya saa 24 kwa ushahidi wa picha,”amesema.
  Aidha, amesema kwamba Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limeiamuru klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia iilipe Simba SC dola 300,000 za Kimarekani za manunuzi ya mshmbauliaji Emmanuel Okwi, lakini wanashindwa kufuatulia kwa sababu TFF haiwasikilizi tena.
  “Kwa kweli tupo wakati mgumu mno, tunashindwa hata kuelewa tunacheza hii ligi kwa sababu gani, inaonekana tunawasindikiza watu ambao tayairi wameandaliwa kwa namna yoyote wawe mabingwa,”amesema.
  Ni kweli TFF kumesheheni watu wa Yanga SC, ambao kiitikadi ni wapinzani wa jadi wa Simba SC.
  Lakini haya ni mambo ya mpito tu, kuna wakati ofisi kuu za soka Tanzania zilisheheni watu wa Simba SC na kuna wakati Yanga SC walilalamika kutotendewa haki.
  Lakini pamoja na ukweli huo, lazima tukubali huu si mfumo bora wa kuongoza soka yetu na tukiendelea hivi tutarudi enzi zile za migogoro kila kukicha.
  Leodegar Tenga, Rais aliyemtangulia Malinzi TFF, pamoja na yote ni kweli kwamba alifanya kazi nzuri ya kujenga mfumo bora wa uongozi ndani ya shirikisho na kuifanya TFF iwe taasisi yenye kuheshimka.
  Tusikubali kuuangusha msingi huu kwa urahisi tu, bali ni vyema tukauimarisha kwa ustawi wa soka yetu.
  Malalamiko ambayo wanatoa Simba SC yanaonekana yana ukweli ndani yake- kwa sababu wanaomba TFF ionyeshe barua moja tu iliyowajibu mwaka huu.
  Kutokujibu kabisa ni dharau, na hatuwezi kuongoza soka ya nchi hii kwa misingi ya kudharauliana. Huu si utaratibu mzuri.
  Si wajibu wa Malinzi kujibu barua, kwa sababu hiyo ni shughuli ya Katibu wake, lakini inapofikia hivi si vibaya akahoji, kwa nini Simba SC hawajibiwi barua zao?
  Wajibiwe ili wajue wamekwama wapi, lakini kitendo cha kutia kapuni barua zao kinawafikisha hapa, wanaona hawatendewi haki na wanapoteza imani na shirikisho.
  Kwa sasa ni viongozi ndiyo wanasema, lakini imani hii ikiwaingia na mashabiki wa timu hiyo itakuwa hatari, maana itakuwa vigumu kuhimili mihemuko yao.
  Kama yupo mtu mmoja ndani ya TFF ana tatizo na mtu mmoja wa Simba SC, basi wote wasitumie vyombo hivyo kwa maslahi au mapambano yao binafsi.
  TFF ni baba wa soka ya Tanzania na Simba SC ni klabu ya wananchi, viongozi wanapewa dhamana ya muda ya kusimamia na wakati ukifika wanatoka, wanaingia wengine.
  Haiyumkiniki eti mwaka wote huu Simba SC hawajajibiwa barua yao yoyote waliyoandika TFF- na leo walete malalamiko yao nasi tuyapuuze. Si sahihi. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MALALAMIKO HAYA YA SIMBA SC NI YA KUFANYIWA KAZI, HAWATENDEWI HAKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top