• HABARI MPYA

  Tuesday, October 20, 2015

  SIMBA SC KUENDELEA KUMKOSA KIZZA ‘DIEGO’ DHIDI YA PRISONS KESHO SOKOINE

  RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA
  Oktoba 21, 2015
  Yanga SC Vs Toto Africans
  Stand United Vs Majimaji FC
  JKT Ruvu Vs Mtibwa Sugar
  Prisons Vs Simba SC
  Coastal Union Vs Kagera Sugar
  Oktoba 22, 2015
  Ndanda FC Vs Azam FC
  Mwadui FC Vs Mgambo Shooting
  Mbeya City Vs African Sports
  Hamisi Kizza ataendelea kukosekana Simba SC kesho ikimenyana na Prisons

  Na Princess Asia, MBEYA
  SIMBA SC itaendelea kumkosa kinara wake wa mabao, Mganda Hamisi Kizza ‘Diego’ katika mechi ya tatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho.
  Simba SC watacheza mechi yao ya pili na ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mjini Mbeya kesho watakapomenyana na wenyeji Prisons Uwanja wa Sokoine.
  Na mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Kizza pamoja na kwamba sasa ameanza kufanya mazoezi kikamilifu, lakini bado analalamika kusumbuliwa na maumivu.
  Kocha Muingereza Dylan Kerr haoni umuhimu wa kumhatarisha Kizza kuumia zaidi katika mchezo wa kesho, hivyo ataendelea kumpumzisha.
  Kizza aliumia nyama mazoezini wiki mbili zilizopita na tangu hapo amejaribu kurudi uwanjani mapema bila ya mafanikio- lakini sasa kuna uhakika mwishoni mwa wiki atakuwa tayari kucheza.   
  Simba SC iliyovuna pointi tatu Jumamosi kutokana na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City, kesho inataka kukamilisha biashara kwa kuwaadhibu na Prisons pia.
  Mchezo wa kesho, safu ya ushambuliaji ya Simba SC itaendelea kumtegemea Nahodha Mussa Hassan Mgosi na Ibrahim Hajib, ambaye msimu huu hadi sasa hajaonyesha cheche. 
  Kwa ujumla, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho, Yanga SC wakiwakaribisha wanawe Toto Africans Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stand United na Majimaji FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, JKT Ruvu na Mtibwa Sugar Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Prisons na Simba SC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Coastal Union na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumatano.
  Ligi Kuu itaendelea tena Alhamisi, Ndanda FC wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mwadui FC ikimenyana na Mgambo Shooting Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati Mbeya City watakuwa wenyeji wa African Sports ya Tanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUENDELEA KUMKOSA KIZZA ‘DIEGO’ DHIDI YA PRISONS KESHO SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top