• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 23, 2015

  SAMATTA NA ULIMWENGU WAAMINI FAINALI ZA LIGI YA MABINGWA ZITAWAPA MAKALI YA KUWAKABILI ALGERIA, LAKINI WASHAURI…

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WASHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Emmanuel Ulimwengu na Mbwana Ally Samatta wanaamini mechi mbili za fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya USM Algier zitawajenga vizuri kuelekea mchezo kati ya Tanzania na Algeria. 
  USM Algier watakuwa wenyeji wa Mazembe Oktoba 30 au Novemba 1, mwaka huu katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana Novemba 8 mjini Lubumbashi.
  Na baada ya hapo, Samatta na Ulimwengu watajiunga na kambi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia Novemba 14, Dar es Salaam na Novemba 17 Algiers.
  Thomas Ulimwengu akifurahia na Mbwana Samatta (10) baada ya kufunga dhidi ya Malawi mapema mwezi huu

  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwa simu kutoka Lubumbashi, Ulimwengu amesema kwamba anaamini mechi hizo mbili dhidi ya USM Algier zitawajenga vizuri kuelekea mechi na Algeria.
  “Mchezo utakuwa mgumu (dhidi ya Algeria), tunaomba Watanzania wajitokeze kutupa sapoti tuweze kupata matokeo mazuri, sisi tunajiandaa vizuri na kwa sababu tuna mechi mbili za fainali (Ligi ya Mabingwa) naona yatakua maandalizi mazuri kwetu kuelekea mechi ya Algeria,”amesema.
  Aidha, Ulimwengu ameshauri pia wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wanacheza ligi ya nyumbani wapatiwe maandalizi mazuri ili nao wawe vizuri kabla ya mchezo huo.
  “Mimi nashauri tujipange vizuri, kwa sababu tunakuja kucheza na namba timu moja kwa ubora Afrika, mechi itakuwa ngumu sana, kocha najua anajua afanye nini kuandaa wachezaji kuelekea mchezo huo, cha msingi umakini uongezeke katika kila jambo ambalo linaelekezwa,”amesema.
  Kwa wachezaji wenzake, Ulimwengu amewashauri kuongeza umakini katika kumsikiliza kocha. “Na viongozi najua wanafahamu umuhimu wa mechi, hivyo tuna imani kubwa mambo yataenda sawa,”ameongeza.
  Ulimwengu pia ameshauri kambi ya nje nchi angalau kwa wiki moja ili kuwajenga vizuri zaidi wachezaji, akiamini mchezo huo utakuwa mgumu kuliko uliopita dhidi ya Malawi. 
  “Ni mechi kubwa, itakua siyo ya kulinganisha na Malawi, kunahitajika umakini mkubwa tuweze kupata matokeo mazuri na kuwaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti, kwa sababu shabiki huwa anakuwa mchezaji wa 12 uwanjani,”amesema.
  Baada ya kuitoa Malawi kwa jumla ya mabao 2-1, wakishinda 2-0 Dar es Salaam mabao ya Ulimwengu na Samatta na kufungwa 1-0 Blantyre, Taifa Stars watakutana na Algeria katikati ya mwezi ujao katika hatua ya mwisho ya kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la 2018 Urusi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA NA ULIMWENGU WAAMINI FAINALI ZA LIGI YA MABINGWA ZITAWAPA MAKALI YA KUWAKABILI ALGERIA, LAKINI WASHAURI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top