• HABARI MPYA

  Tuesday, October 27, 2015

  YANGA SC KUIVAA MWADUI FC BILA TELELA KESHO

  Salum Telela atakosekana kesho dhidi ya Mwadui FC kutokana na maumivu ya kifundo cha mguu
  Na Prince Akbar, SHINYANGA
  YANGA SC itamkosa kiungo wake Salum Abdul Telela ‘Master’ katika mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya Mwadui FC, Uwanja wa Kamabrage, Shinyanga.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE jioni ya leo kwamba, Telela amebaki Dar es Salaam kwa sababu ya matibabu ya kifundo cha mguu.
  Mbali na Telela, Muro amesema kipa wao wa tatu, Mudathir Khamis naye hatakuwepo katika mchezo huo, kwa sababu amekwenda kwao Zanzibar kwa matatizo ya kifamilia.
  Pamoja na kukosekana kwa wachezaji hao wawili, Muro amesema kikosi kilichopo mjini Shinyanga tangu jana kwa ajili ya mchezo wa kesho kinatosha.
  “Uzuri ni kwamba tuna wigo mpana wa wachezaji na wote bora, hata wanaposekana wengine kadhaa, wanaobaki wanatosha kabisa kuleta ushindi,”amesema.
  Muro amesema timu imefanya mazoezi yake ya mwisho leo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na wachezaji wote wako fiti tayari kuvuna pointi tatu kesho.
  Amesema mashabiki wa Stand United, ambao ni mahasimu wa Mwadui FC wameipokea Yanga SC vizuri na wameahidi kuishangilia kesho ili iwafunge wapinzani wao wa mkoa wa Shinyanga.
  Kwa ujumla, Ligi Kuu inaendelea kesho, mbali na Mwadui FC na Yanga SC Uwanja wa Kambarage, Toto Africans watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Simba watakuwa wenyeji wa Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa ndugu zao Kagera Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro. 
  Mbeya City watakuwa wenyeji wa Majimaji FC Uwanja wa Sokoine, Ndanda FC wataikaribisha Stand United Uwanja wa Nangwanda, Mtwara wakati kesho JKT Ruvu watamenyana na Azam FC Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na Prisons wataikaribisha African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC KUIVAA MWADUI FC BILA TELELA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top