• HABARI MPYA

  Wednesday, October 28, 2015

  SAMATTA NA ULIMWENGU WAPELEKWA ‘KOZI YA KUUWA’ WAALGERIA

  KLABU ya TP Mazembe imeweka kambi mjini Marrakech, Morocco tangu Jumapili usiku kujiandaa na fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya USM Alger mwishoni mwa wiki nchini Algeria.
  Saa kadhaa tu baada ya sare ya 1-1 na Bazano katika mchezo wa ligi ya DRC, The Ravens walikwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luano kupanda ndege Saa 3: 45 usiku kwenda Morocco.
  Wachezaji 24, wakiwemo washambuliaji tegemeo, Watanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wako mjini Marakech wanajifua vikali. 
  Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ni wachezaji tegemeo Tanzania

  Mazembe iliyofikia katika hoteli ya hadhi ya nyota tano, Golf Hotel, ilianza mazoezi juzi mjini Marakech na inatarajiwa kuhitimisha kambi yake hiyo Alhamisi kabla ya safari ya Algiers Ijumaa kwa mchezo huo.
  USM Algier watakuwa wenyeji wa Mazembe katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana Novemba 8 mjini Lubumbashi.
  Na baada ya hapo, Samatta na Ulimwengu watajiunga na kambi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars nchini Oman kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia Novemba 14, Dar es Salaam na Novemba 17 marudiano Algiers.
  Ulimwengu na Samatta wanaamini mechi hizo mbili dhidi ya USM Algier zitawajenga vizuri kuelekea mechi na Algeria.
  “Mchezo utakuwa mgumu (dhidi ya Algeria), tunaomba Watanzania wajitokeze kutupa sapoti tuweze kupata matokeo mazuri, sisi tunajiandaa vizuri na kwa sababu tuna mechi mbili za fainali (Ligi ya Mabingwa) naona yatakua maandalizi mazuri kwetu kuelekea mechi ya Algeria,”alisema Ulimwengu.
  Aidha, Ulimwengu ameshauri pia wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wanacheza ligi ya nyumbani wapatiwe maandalizi mazuri ili nao wawe vizuri kabla ya mchezo huo.
  “Mimi nashauri tujipange vizuri, kwa sababu tunakuja kucheza na timu namba moja kwa ubora Afrika, mechi itakuwa ngumu sana, kocha najua anajua afanye nini kuandaa wachezaji kuelekea mchezo huo, cha msingi umakini uongezeke katika kila jambo ambalo linaelekezwa,”amesema.
  Kwa wachezaji wenzake, Ulimwengu amewashauri kuongeza umakini katika kumsikiliza kocha. “Na viongozi najua wanafahamu umuhimu wa mechi, hivyo tuna imani kubwa mambo yataenda sawa,”ameongeza.
  Baada ya kuitoa Malawi kwa jumla ya mabao 2-1, wakishinda 2-0 Dar es Salaam mabao ya Ulimwengu na Samatta na kufungwa 1-0 Blantyre, Taifa Stars watakutana na Algeria katikati ya mwezi ujao katika hatua ya mwisho ya kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la 2018 Urusi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA NA ULIMWENGU WAPELEKWA ‘KOZI YA KUUWA’ WAALGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top