• HABARI MPYA

  Sunday, October 25, 2015

  HAWA MAKOCHA WA SIMBA NI KIBOKO, POLE YAO MSIMBAZI!

  AGOSTI 16, mwaka huu katika safu yangu hii niliandika makala yenye kichwa; “HII YA KOCHA WA SIMBA NA MAGURI TUFUNIKE TU KOMBE ‘MWANAHARAM’ APITE, NDIYO MACHUNGU YENYEWE!”
  Nilianzia mbali kidogo, nikielezea machungu ambayo wanakutana nayo wanasoka mfano kilio cha mshambuliaji wa zamani wa kimataifa nchini, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ au ‘Bonga Bonga’ ambaye miaka mitatu iliyopita alikaribia kunitoa machozi.
  Ilikuwa ni katikati ya mjadala wa maisha ya wanasoka wengi baada ya soka na Bonga akasema; “Kama ningejua, ningejibidiisha kwenye shule tu, leo ningekuwa na kazi yangu ninaishi vizuri,”.

  Nilimuelewa Bonga. Alianza kuwika kisoka akiwa kijana wa umri chini ya miaka 20, maana yake alianza kujifunza soka bado mdogo sana. Maana yake hakuwa na muda wa kusoma shule.
  Akafanikiwa kisoka, akacheza klabu kubwa, Yanga SC na timu ya taifa, taifa Stars- lakini bahati mbaya, wakati ambao anacheza, hakukuwa na fedha. Ulikuwa wakati wa soka ya ridhaa.
  Soka ya Ridhaa malipo yake yalikuwa umaarufu na nje ya Uwanja, malipo ya ziada yalikuwa kupata ofa za pombe na wanawake wa ‘bure bure’ wapenda ‘mastaa’.
  Nikakumbushia pia mahojiano yangu na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima miaka mitano iliyopita anakuja Tanzania. Nilimuuliza Haruna angependa mwanawe naye acheze soka, akasema; “Hapana”.
  Nilipomuuliza kwa sababu gani, akajibu; “Soka ni mchezo wenye machungu mengi sana, nisingependa mwanangu apitie machungu hayo, nataka asome aje kuwa na elimu yake nzuri, aishi kwa furaha na amani,”.
  Sahau kuhusu hayo ya Bonga, soka umeendelea kuwa mchezo wenye changamoto nyingi na machungu pia, hususan kwa huku kwetu Tanzania.
  Huku kwetu ndiko wachezaji wanatolewa ‘kafara’ kuficha mapungufu ya uongozi. Mchezaji anaambiwa amehujumu timu na akafukuzwa bila kupewa haki zake.
  Kidogo kwa mfumo wa sasa, tumeondoka huko. Sasa wakifukuzwa, wenye kuweza kufuatilia haki zao, wanapata.
  Wanasema siri ya mafanikio ni bidii ya mazoezi nidhamu na kujituma- lakini si kila anayefanya hivyo hufanikiwa.
  Kocha mpya wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr alimtema mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Elias Maguri baada ya kumjaribu katika mechi nne akifunga mabao matatu, kwa madai kwamba mchezaji huyo anakosa sana mabao.
  Maguri alifunga bao moja kila mechi katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Black Sailor, 3-0 dhidi ya Jang’ombe Boys na 2-1 dhidi ya Polisi Zanzibar.
  Kerr alimtumia Maguri katika mechi nne kwenye kambi ya visiwani Zanzibar Agosti mwaka huu na mchezaji huyo akafunga mabao matatu, lakini haikumsaidia kumshawishi Muingereza huyo.
  Kerr akawaambia viongozi wa Simba SC waachane na mchezaji huyo hamuhitaji katika kikosi chake.
  Sababu? Kerr akawaambia viongozi wa Simba SC kwamba mchezaji huyo anapoteza nafasi nyingi za kufunga mabao.
  Na akasema kwamba ana vijana wengi wa kikosi cha vijana, Simba B ambao anaweza kuwatayarisha kuwa washambuliaji wazuri kuliko Maguri.
  Lakini uongozi ukamuambia, mchezaji huyo bado ana Mkataba wa mwaka mzima, hivyo akiachwa klabu italazimika kumlipa- na Kerr akawajibu; “Hata akibaki, hatacheza, atakuwa anafanya mazoezi tu,”.
  Baada ya yote hayo, uongozi wa Simba SC ukakutana na Maguri na kumshauri atafute timu ya kucheza kwa mkopo kwa miezi sita ili kurudisha kiwango chake, labda anaweza kurejeshwa Msimbazi.
  Sijui kiwango kipi walitaka arudishe, wakati alikuwa anafunga karibu kila mechi na alifunga pia dhidi ya watani, Yanga SC.
  Maguri hakutaka kuondoka kwa mkopo, aliamua kumalizana moja kwa moja na Simba SC na akaondoka akiwa mchezaji huru.
  Akajiunga na Stand United ya Shinyanga na sasa katika chati ya wafungaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Maguri anaongoza kwa mabao yake nane, akifuatiwa kwa mbali na Donald Ngoma, Amissi Tambwe wote wa Yanga, wenye mabao matano kila mmoja sawa na 
  Hamisi Kiiza wa Simba SC na Kipre Tchetche wa Azam FC.
  Katika kipindi cha mwaka mmoja cha Maguri kuichezea Simba SC, amefunga mabao 12 katika mechi 43 za mashindano yote, zikiwemo za kirafiki tena nyingi akitokea benchi.
  Simba SC ilimsajili Maguri kutoka Ruvu Shooting baada ya kushika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu msimu wa 2013/2014 na wakati huo huo akiwa tayari ameanza kuitwa timu ya taifa, chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen. 
  Kabla ya kumpata Kerr, Simba SC ilijaribu kumchukua Kim, lakini wakashindwana- maana yake kama Mdenmark huyo angetua Msimbazi, Maguri asingetemwa Msimbazi.
  Nilisema; ninamuheshimu Kerr, lakini pia ninamuhesimu Kim. Na pia ninamuheshimu kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Tom Olaba aliyempa nafasi Maguri Ruvu Shooting hadi akawa mfungaji bora namba tatu katika Ligi Kuu, kiasi cha Simba kumpenda na kumsajili.
  Nilisema Agosti 16 mwaka huu kwamba maamuzi ya Kerr, tufunike kombe ‘mwanaharam’ apite, lakini Simba inapoteza mshambuliaji na mfungaji mzuri wa mabao.
  Leo miezi miezi miwili na ushei baadaye, Maguri anawadhihirishia Simba SC walifanya makosa kumuacha. Na bahati mbaya sana, kocha Mfaransa, Patrick Liewig hakumpanga Maguri katika mechi dhidi ya Simba SC Dar es Salaam, bila shaka angewachoma roho zaidi kama angewafunga.  
  Kwa Simba SC haya ni maumivu mengine, baada ya kumuacha mshambuliaji mwingine mzuri kwa kufunga msimu uliopita, Amissi Tambwe ambaye amehamia kwa mahasimu, Yanga SC.
  Tambwe aliachwa Simba SC akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu, ikidaiwa kocha Mzambia Patrick Phiri ndiye aliyependekeza, akisema mchezaji huyu haendani na mipango yake.
  Hapo unazungumzia wafungaji, lakini hivi karibuni Simba SC imepoteza wachezaji wengi wazuri wakiwemo vijana wadogo kwa sababu ambazo hazieleweki.
  Amri Kiemba na Haroun Chanongo wote waliachwa Simba ya Phiri wakiwa wachezaji wa timu ya taifa- bado kuna chipukizi wengine kama Miraj Athumani ‘Madenge’, Hassan Khatib, Edward Christopher ambao wote sasa wanaendelea kufanya vizuri timu nyingine.
  Lakini wote wanapoachwa, inaelezwa ni mapendekezo ya makocha na haijawahi kutokea kocha yeyote akakana. Mfano hili la Maguri, Kerr hajakana kwamba ndiye aliyependekeza aachwe. Sasa tujulize Simba SC inapata makocha wa aina gani siku hizi?
  Nauona mwanzo wa mwisho wa mshambuliaji mwingine mzuri chipukizi Simba SC, Ibrahim Hajib ambaye baada ya kuibuka vizuri msimu uliopita, nafasi yake uwanjani chini ya Kerr inaanza kupungua taratibu.
  Na ninaona dalili za Simba SC kuachana na Muingereza huyo baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu- tu kwa ushauri wake mbaya katika usajili, ukiachilia mbali na matokeo.
  Tayari Simba SC imepoteza mechi mbili kati ya saba ilizocheza, wakati wapinzani Yanga na Azam FC wameshinda zote na sare moja kila mmoja, maana yake ndoto za ubingwa Msimbazi zinaanza kuyeyuka taratibu.
  Unaizungumzia timu ambayo ina miaka mitatu haiajashika hata nafasi ya pili katika Ligi Kuu, maana yake kipindi chote hicho haijacheza michuano ya Afrika.
  Simba SC ni wa kupewa pole tu, maana makocha wanaowapata siku hizi ni kiboko!
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAWA MAKOCHA WA SIMBA NI KIBOKO, POLE YAO MSIMBAZI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top