• HABARI MPYA

  Wednesday, October 21, 2015

  'MAPOVU' YANAWATOKA BURE, HAKUNA KAMATI YA KUIFUNGA ALGERIA

  WAKATI wote timu yetu ya taifa inapofanya vibaya, sisi wa vyombo vya Habari tumekuwa mstari wa mbele kulaumu maandalizi na mikakati dhaifu.
  Kwa muda viongozi wetu wa soka wamekuwa wakipuuzia maoni na mitazamo ya wadau na tumekuwa tunaendelea na staili ya bora liende.
  Safari hii, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeunda Kamati maalum, inayokutanisha wadau wa aina tofauti wakiwemo wa vyombo vya habari.
  Tayari Kamati hiyo imekutana na kuunda Kamati nyingine ndogo ndogo kuelekea mchezo na Algeria katikati ya mwezi ujao kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia. 

  Kamati Kuu ya Taifa Stars iliyoteuliwa na TFF, inaundwa na Mwenyekiti Farough Baghozah, Makamu wake, Michael Wambura, Katibu Teddy Mapunda, Mweka Hazina Wakili Imani Madega na Wajumbe Juma Pinto, Isaac Chanji, Salum Abdallah na Musa Katabaro.
  Kamati hiyo imeunda kamati ndogondogo ambazo ni Maandalizi ya timu, chini ya Mwenyekiti Wakili Madega na Wajumbe Ahmed Mgoyi, Teddy Mapunda, Kamati ya 
  Uhamasishaji wa mechi na Masoko chini ya Mwenyekiti Juma Pinto na Wajumbe Baraka Kizuguto, Mulamu Ng’ambi, Charles Hamka, Hashim Lundenga, Maulid Kitenge, Shaffih Dauda, Salehe Ally, Peter Simon, Edo Kumwembe na Mahmoud Zubeiry.
  Pia kuna Kamati ya Fedha, chini ya Baghozah mwenyewe na Wajumbe – Teddy Mapunda, Michael Wambura, Imani Madega, Juma Pinto, Isaac Chanji, Moses Katabaro na Edgar Masoud.
  Kuna Kamati ya Mikakati ya ushindi inayoundwa na Mwenyekiti Farough Baghozah, Teddy Mapunda, Mohamed Nassoro, Philemon Ntahilaja, Isaac Kasanga, Crescencius Magori.
  Kamati imetangaza kauli mbiu ya ushindi inayosema “NCHI YETU, TIMU YETU, TAIFA LETU, USHINDI WETU” iliyoanza kutumika mara moja.
  Katika Kamati hizi, Hakuna Kamati inayoitwa ya kuifunga Algeria- kuna Kamati mbalimbali zenye majukumu tofauti.
  Lengo ni kuhakikisha kunakuwa na maandalizi madhubuti katika kila eneo kabla ya mchezo kwa mujibu wa uzoefu wa mashindano ya aina hii.
  Na TFF inataka hata kama timu ikitolewa, basi Watanzania waridhike jitihada zilifanyika kuliko kujikatia tamaa mapema.
  Ni kama tu ilivyounda Kamati ya Soka la Ufukweni ambayo timu yake ilifungwa ‘hadi aibu’ na Misri nyumbanina ugenini.
  Pamoja na hayo, kumeibuka kama uasi fulani na kuna Redio moja yenyewe imekuwa ikipiga vita kila kukicha kuhusu Kamati. Inaponda tu, tena bila sababu. Kama ina chuki hivi. Na sijui ni chuki za nini.
  Huu ni upungufu mkubwa, wakati mwingine ni vyema kuelewa dhana kuliko kupayuka na kuzomoka kama juha- ni kutaka sifa, au kitu gani?
  Hakuna Kamati ya kuifunga Algeria, kuna Kamati za maandalizi ya mchezo dhidi ya Algeria- kama huna shaka na Utanzania wako unaweza kujiunga na kampeni.
  Wote tunafahamu Algeria ni bora kuliko Tanzania na ni bora kuliko nchi zote za Afrika, lakini kama kweli mtu wa soka huwezi kuwa na mawazo mgando eti Taifa Stars imekwishatolewa.
  Senegal iliifunga Ufaransa bora mwaka 2002 katika Kombe la Dunia, lakini sisi tu Tanzania mara ngapi tumeanguasha vigogo hapa?  
  Tanzania ilikuwa ina ubora gani wakati inaifunga Morocco 3-1 hapa Dar es Salaam mwaka juzi?
  Sioni mantiki ya kila kukicha kushambulia Kamati ya Taifa Stars, ambayo masikini Wajumbe wake wanakwenda kwenye vikao kwa gharama zao na hawalipwi posho, wanajitolea kwa uzalendo wao tu. Niishie hapa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: 'MAPOVU' YANAWATOKA BURE, HAKUNA KAMATI YA KUIFUNGA ALGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top