• HABARI MPYA

  Saturday, October 31, 2015

  SIMBA SC YACHARUKA, YAITANDIKA MAJIMAJI 6-1 TAIFA, HAJIB APIGA TATU, KIZZA MAWILI

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Ibrahim Hajib ‘Kadabra’ amefunga mabao matatu peke yake, Simba SC ikishinda 6-1 dhidi ya Majimaji ya Songea katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Hiyo inakuwa hat trick ya pili katika Ligi Kuu msimu huu na zote zikitoka Simba SC, baada ya awali Mganda Hamisi Kizza kufanya hivyo.
  Na ushindi huo, unaifanya timu ya kocha Muingereza Dylan Kerr ifikishe pointi 21 baada ya kucheza mechi tisa, ikiendelea kushika nafasi ya nne nyuma ya Yanga SC, Azam FC na Mtibwa Sugar. 
  Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza hajib baada ya kupiga hat trick leo

  Ibrahim Hajib alifunga mabao mawili ndani ya dakika nne, la kwanza dakika ya nane kwa shuti akimalizia pasi ya kiungo Justice Majabvi na la pili dakika ya 11 kwa kichwa akimalizia krosi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Mganda Hamisi Kizza ‘Diego’ akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 37 kwa shuti akimalizia krosi ya Tshabalala.
  Hajib akakamilisha hat trick yake dakika ya 42 akimalizia kwa kichwa krosi ya kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula.
  Kipindi cha pili, Simba SC waliendelea kuitesa Majimaji baada ya kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi yaliyofungwa na Tshabalala dakika ya 78 na Kizza dakika ya 81, ambalo linakuwa bao lake la nane msimu huu. 
  Ditram Nchimbi aliifungia bao la kufutia machozi Majimaji dakika ya 88.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Jonas Mkude/Joseph Kimwaga dk66, Awadhi Juma, Mwinyi Kazimoto, Hamisi Kizza, Ibrahim Hajib/Pape N'daw dk75 na Peter Mwalyanzi/Simon Sserunkuma dk85. 
  Majimaji FC: David Burhan, Freddy Mbuna, Ally Mohammed/Godfrey Taita dk46, Peter Joseph, Samir Ruhava, Sadiq Gawaza, Hassan Hamisi, Frank Sekule, Idd Kipagwile, Ditram Nchimbi na Stahmil Mbonde.
  Mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Hajib akimtoka bekiwa Majimaji FC, Ally Mohamed leo
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YACHARUKA, YAITANDIKA MAJIMAJI 6-1 TAIFA, HAJIB APIGA TATU, KIZZA MAWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top