• HABARI MPYA

    Tuesday, April 14, 2015

    PIGA, UA SOKA YA TANZANIA NI SIMBA NA YANGA TU, AZAM WASIPOKAZA BUTI ITAKULA KWAO

    Na George Mganga, DAR ES SALAAM
    UKIFUMBA macho na kuangalia miezi takribani sita au saba iliyopita, unaweza leo hii ukabaki mdomo wazi.
    Kipindi hiko Mtibwa Sugar ilikuwa inaongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na ndicho kipindi ambacho kocha chipukizi, Mecky Mexime
    alikuwa anaonekana bora hadi wenye ‘matege’ ya kufikiri wakawa wanapendekeza apewe timu ya taifa. Na mwenyewe Mexime ndicho kipindi ambacho alikuwa ‘anaropoka hovyo’ na hata kufikia hatua kuwaponda makocha wenzake, lakini wachache tulibaki tu kumsikiliza na kujiuliza, kwa ukocha gani alionao? 
    Lakini hivi tunavyozungumza, Mtibwa inapigania kuepuka kushuka daraja na mdomo wa Mexime kama una kazi kubwa zaidi ya kufanya ni kubugia matonge ya ugali kuliko kuzungumza.
    Wachezaji wa Simba na Yanga wakigombana katika moja ya mechi baina yao

    Lakini pia, ukifumba macho na kuiangalia ligi ya msimu uliopita, utaona jinsi ambavyo Mbeya City walivyoleta ‘amsha amsha’ katika soka ya Tanzania.
    Staili yao ya kurudisha wanachokipata kwa wananchi wahitaji, mashabiki wao kwa kwenda mahospitalini kuwaona na kuwafariji wagonjwa na mwisho wa siku waliweza
    kujitolea kufanya usafi katika jiji lao, watu tukasema sasa timu ya kijamii imepatikana.
    Lakini kilichotea hivi sasa, kila mtu anashika kichwa. Walianza kutimuana wenyewe kwa wenyewe, siasa za kimkoa zikawatafuna hatimaye wamepotea na usishangae msimu ujao tukawakuta wakiwa katika nafasi ya kupigania kutoshuka daraja.Haya siyo mapya kwa sisi tuliokula chumvi nyingi kidogo, kuyaona katika ligi ya Tanzania. Kulikuwepo na timu nyingi tu za aina hii, kwa kawaida timu kama hizi, tunaziita "timu mlipuko".
    Walikuwepo Kajumulo WS, chini ya umiliki wa Mmarekani mwenye asili ya Bukoba, Tanzania, Alexander Otaqs Kajumulo, Tukuyu Stars, Pallsons chini ya Thomas Mollel ‘Askofu’ na wote wamepotea na timu zao.
    Nini shida? Tatizo kubwa linaloziathiri timu hizi
    mlipuko ni moja tu, nalo ni malengo yao ya kuwepo Ligi Kuu siku zote hayawi katika
    kuchukua Kombe, bali kushindana na Yanga na
    Simba. Hapo ndipo wanapoanza wenyewe kujipoteza.
    Ukiiangalia Azam FC, utaona kama ni klabu ambayo ipo kisasa zaidi. Ni kweli, ina kila kitu tena kuzishinda klabu nyingi Afrika na muda mwingine hata ulaya kwenyewe. Lakini zaidi ya kuchukua
    Kombe la Ligi Kuu nini kingine cha kujivunia kwao?
    Malengo ya uanzishwaji wa Azam yalikuwa yapi?
    Kwanza ieleweke, Azam ni chimbuko la timu ya wafanyakazi wa Bakhresa Group Limited, ambao waliamua kuunda timu yao kwa ajili ya kujifariji baada ya kazi.
    Mwisho wa siku waliamua kununua haki za Kipawa FC, na rasmi kuanza kushiriki ligi ya Mkoa, wakipanda taratibu hadi Ligi Kuu mwaka 2008.
    Niwapongeze Azam FC kwa kufanikiwa kwa miaka mitatu mfululizo kuitupa nje ya timu mbili za juu kwenye Ligi, ama Simba au Yanga, huku pia ikichukua ubingwa mara moja, msimu uliopita.
    Mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche akimtoka beki wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala' 

    Azam imeshika nafasi ya pili mara mbili, kwanza nyuma ya Simba, baadaye nyuma ya Yanga na msimu uliopita ikawa bingwa ikifuatiwa na Yanga.   
    Azam FC imeikosesha Simba SC kucheza michuano ya Afrika mara mbili, mwaka jana na mwaka huu. Lakini baada ya kutisha kwa misimu mitatu mfululizo, Azam FC inaonekana kulegalegaa na picha inayoonekana sasa, itakuja kugombea nafasi ya pili ya na sahiba zao, Simba SC.  
    Nani asiyejua Simba SC na Azam wanapikika chungu kimoja? Ndiyo maana wanabadilishana wachezaji, wanapeana dili za hapa na pale- mambo ambayo hayawezekani kutokea baina yao na Yanga.
    Lakini pamoja na yote, Simba SC wanataka kurudi Afrika na wamekwishatamka kupitia Mwenyekiti wao wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe kwamba wanaitaka nafasi ya pili. Maana yake wanataka kuitoa Azam FC.
    Kwa aina ya uwekezaji ambao Azam FC imefanya ni hatari sana ikikosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani, lakini watafanya nini na soka ya Tanzania ni ya Simba na Yanga tu? 

    (Mwandishi wa makala haya ni mpenzi na msomaji wa BIN ZUBEIRY ambaye anapatikana kwa namba +255 688 665 508)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PIGA, UA SOKA YA TANZANIA NI SIMBA NA YANGA TU, AZAM WASIPOKAZA BUTI ITAKULA KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top