• HABARI MPYA

    Tuesday, April 07, 2015

    MIAKA 43 TANGU KIFO CHAKE; MAJENGO YA SIMBA NA YANGA PEKEE YATOSHA KARUME AKUMBUKWE DAIMA

    Na Masoud Sanani, ZANZIBAR
    LEO Aprili 7 Watanzania wanakumbuka kifo cha aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume aliyeuawa kwa kupigwa risasi siku hiyo mwaka 1972. Ni miaka 43 sasa kifo chake.
    Mzee Karume atakumbukwa kwa mengi enzi za uhai wake, ikiweko kuzisaidia fedha klabu za Simba na Yanga kuwa na majengo yake, pale Msimbazi (Simba SC) na Jangwani (Yanga SC).
    Na ni Karume aliyefanya Simba SC waachane na jina la Sunderland, akiamini kufanya hivyo ni kuutukuza ukoloni. Alikuwa mpendamichezo, lakini alichukia michezo ya kujeruhiana, akiamini ni ya kitwana.
    Ndiyo maana alizuia mchezo wa ngumi Zanzibar na hadi leo hauchezwi. Aliifundia timu ya Mwadui ya Shinyanga kucheza Zanzibar kwa sababu ya rafu mbaya.
    Mwandishi nguli wa habari za michezo Tanzania, MASOUD SANANI anazungumza na mjane wa Mzee Karume, Mama Fatma Karume juu ya Mzee Karume na masuala mengine kadhaa. Mwanamke huyo mcheshi na mwenye bashasha anajibu maswali ya mwandishi kama ifuatavyo.
    Hayati Abeid Amaan Karume atakumbukwa daima na wanamichezo

    Swali: Mama Fatma mlikutana wapi na Mzee Karume na ilikuwaje hadi mkawa mume na mke?
    Jibu: Mzee Karume alikuwa mtu wa kusafiri kwenda Ulaya mara nyingi. Aliporudi hapa akaunda kikundi cha kupiga muziki wa dansi kilichoitwa African Dancing Club pale Michezani. Wakati huo kulikuwa hakuna bendi wakawa wanapiga santuri, vijana wakawa wanacheza.
    Siku zinakwenda, mambo yanafunguka mtu mmoja akiitwa Salum Beni akajitokeza kupiga muziki wakawa wanamkodi. Mara nyingi akawa anawapigia hasa wakati wa kuvunja jungu na sikukuu.
    Akawa maarufu. Akawa anatakiwa kupiga sehemu zingine, sasa huyu Beni akawa anawapiga chenga. Wakamchukua mtu mwingine akiitwa Rashid Kigogo, sasa huyo akawa anawapigia muziki. Huyu Kigogo alikuwa mume wa mama yangu mkubwa alikuwa akiiishi pale Mwembeladu Mbuyupacha. Wakati wa siku za sikukuu nilikuwa nikienda kwa mama mkubwa. Siku moja Mzee Karume alikuja hapo kuongea na Mzee Kigogo akaniona wakati huo nikiwa kijakazi mzima. Akamuuliza mwenyeji wake huyo ni mtoto wa nani? Mzee Kigogo akamjibu ni mwanangu lakini Mzee Karume hakutaka kuamini.
    Akamsisitizia ni mwanangu. Karume akasema anataka kuja kuniposa. Mzee Kigogo akamwambia ili uamini kuwa ni mwanangu nitakuja naye kwenye dansi. Siku hiyo Mzee Kigogo akanichukua kwenye dansi name kwa mara ya kwanza nikawaona watu wakicheza dansi. Mzee Karume akawafuata wazee akaposa na akakubaliwa na baada ya muda akanioa.
    Kila unapolitzama jengo hili la Yanga SC, lazima umkumbuke marehemu Karume
    Karume aliwasaidia Simba SC pia fedha za kujenga jengo lao Msimbazi

    Swali: Harusi yenu ilikuwaje?
    Jibu: Haikuwa harusi kubwa. Shughuli ilifanyika kwetu, Bumbwini. Aliporudi mjini akatuma gari, nakumbuka lilikuwa jeusi, wakati huo si rahisi kwa gari kwenda shamba. Nikachukuliwa nikafikia kwa mama mkubwa nikashinda hapo na usiku nikapelekwa kwangu, Kisimajongoo. Kikundi chake cha African Dancing Club wakafanya sherehe wakapiga dansi hapo nyumbani na wakacheza sana.
    Swali: Maisha mapya yalianza vipi?
    Jibu: Nilikuwa mke wa nyumbani nikatawishwa. Nikapata mimba lakini haikuwa riziki, badaye nikapata mimba ya Amani na baadaye Ali ambao ndiyo watoto wangu pekee wa kuwazaa.
    Mzee Karume alishaoa kabla yangu, lakini bahati mbaya hakujaaliwa kupata watoto. Lakini nilipoolewa mimi hakuwa na mke kwa hiyo sikuwa na mke mwenza.
    Mama Fatma Karume (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein (kulia) iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa ajili ya marehemu mumewe 

    Lakini, alipokuja kuwa Rais alioa wake wengine, wakati ule ziliingia zile ndoa sijui zinaitwaje, viongozi wengi walioa na yeye akaoa na ana watoto wengine watatu, wanajuana na kaka zao na mimi wananijali.
    Awali wakati wa maisha yetu, Mzee Karume alikuwa anafanya kazi bandarini. Walikuwa na ushirika wao wa boti, walikuwa wanasafirisha watu na mizigo. Hiyo ndiyo iliyokuwa kazi yake.
    Swali: Mzee Karume alikuwa ni mtu wa aina gani?
    Jibu: Mzee Karume hakuwa mtu mwenye hasira. Alikuwa mtu wa kupenda watu. Alikuwa na kipaji, lakini zamani tulikuwa hatujui vipaji. Alikuwa mtu bashasha alikuwa akipenda kusaidia watu. Amenifunza mambo mengi na kunikataza mengi.
    Swali: Hali ya sasa unaionaje tangu kifo cha Mzee Karume, malengo aliyoyapanga yamefikiwa?
    Jibu: Kila mtu anapoingia madarakani anakuwa na malengo yake. Alikuwa na mipango ya kuwa na nyumba kama vile Michenzani na nyumba za vijiji. Akajenga sehemu mbalimbali. Sasa tujiulize zile nyumba alizojenga bado zipo? Zimeongezeka au vipi? Nilicho na hakika ni kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bado ipo.
    Swali: Ndoto za Mzee Karume za maendeleo ni kuifanya Zanzibar iwe kama Ulaya, unadhani alifanikiwa?
    Jibu: Alifanikiwa lakini hakupata nafasi ya kumaliza kutekeleza dhamira yake. Angepata nafasi, leo tungekuwa na mengi ya kujivunia. Aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa amekaa madarakani kwa miaka minane tu.
    Swali: Mzee Karume alipenda umoja, mwanawe Amani Karume alikuwa injinia wa kuleta maridhiano Zanzibar akishirikiana na Maalim Seif Sharif Hamad. Lakini, hali inaonekana kuanza kujirudia kama zamani (kabla ya maridhiano) unadhani nini kifanyike?
    Jibu: Kwa upandewa matokeo mabaya na vipeperushi vya matusi na vitisho yanatokea kwa sababu ya utashi wa watu. Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar sijaiona kasoro yake. Matokeo mengine ni kwa utashi wa watu, wengine hawana uvumilivu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MIAKA 43 TANGU KIFO CHAKE; MAJENGO YA SIMBA NA YANGA PEKEE YATOSHA KARUME AKUMBUKWE DAIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top