• HABARI MPYA

    Thursday, January 02, 2014

    UTAMSIFIA KWA LIPI RAMADHANI SINGANO ‘MESSI WA MSIMBAZI’?

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    JANA ilikuwa siku nyingine ya kushuhudia utajiri ulio kwenye mguu wa kushoto wa Ramadhani Singano ‘Messi’, kiungo wa pembeni wa Simba SC.
    Messi aliichezea Simba SC tangu mwanzo katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi, Kundi B dhidi ya AFC Leopard ya Kenya Uwanja wa Amaan, Zanzibar na akatoa krosi iliyozaa bao pekee la ushindi.
    Aliwekewa mpira kwenye njia yake wingi ya kulia na beki Haruna Shamte- na alipoinua sura yake akamuona beki Joseph Shikokoti anamfuata kwa kasi.
    Kipaji; Ramadhani Singano 'Messi' anaweza kuvuna fedha nyingi kutokana na kipaji chake kwa staili yake ya uchezaji kama Robben chini


    Messi akatoka nje zaidi kumvuta beki huyo, akavutika akamkimbiza kidogo, kisha akafunga breki na kumlamba chenga kama tu ile aliyomlamba Kevin Yondan wa Yanga, Desemba 21, mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Lakini tu Shikokoti hakumchezea rafu Messi kama alivyofanya Yondan, aliyepewa kadi ya pili ya njano na Mkenya huyo akamuachia mjukuu wa mzee Sinagano afanya anachokitaka.
    Messi akachungulia ndani namna wachezaji wa Leopard walivyojipanga dhidi ya wachezaji wa timu yake, akamimina krosi maridadi na Amisi Tambwe akaunganisha, lakini ikaokolewa na kumkuta Amri Ramadhani Kiemba, aliyemgeuza beki mmoja wa timu hiyo ya Kenya kabla ya kufumua shuti kwa guu la kushoto lililotinga nyavuni.
    Mbali na kutoa krosi ya bao hilo, Messi aliwahenyesha mno mabeki wa Leopard na kwa ujumla kama kungekuwa kuna tuzo ya mchezaji bora wa mechi, basi dogo huyo angestahili kupewa.
    Messi akiwa na umri wa miaka 20 tu, kwa uwezo na kipaji chake anaweza kucheza popote na kunufaika na kipaji chake kwa malipo mazuri, iwapo atajibidiisha na mazoezi zaidi, ili kuwa fiti zaidi.
    Messi wa Msimbazi akimtoka Shikokoti jana upande wa kulia kabla ya kutia krosi kwa guu lake la kushoto, iliyozaa bao pekee la Simba SC
    Tazama anavyomiliki mpira kwa mguu wa kushoto upande wa kulia, hapa Yondan alipigwa chenga ambayo anaweza asiisahau hadi anastaafu soka

    Kipimo chake ni kwanza kuhakikisha anakuwa mchezaji tegemeo wa Simba SC na anaendelea kuisaidia timu. Pili, awe mchezaji wa kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kuwa tegemeo la timu.
    Akiweza hayo, basi ataanza kumulikuwa na mawakala wa wachezaji kwa lengo la kumpatia timu nje. Kuna kitu kimoja, ambacho wachezaji wengi wa Tanzania hawazingatii- kwamba uwezo unatokana na mazoezi, lakini wengi wao, wanapokuwa mastaa, wanahamishia umahiri kwenye starehe na anasa.
    Mazoezi yanakuwa ya kuvizia vizia, kiburi kinaanza, dharau na ujuaji mwingi- matokeo yake ndani ya muda mfupi wanabaki historia. Wengi tu sasa wanabebwa na majina baada ya uwezo kuwakimbia na kubaki watu wa kulalamika, wenye kudhani wanaonewa, wanalogwa, au hawapendwi.
    Heri yao waliokaa darasani kidogo, watakuja kubangaiza kwenye magazeti kwa kuandika andika uchambuzi, lakini ‘wenzangu na mie’ labda watakwenda kuwa makocha wa soka ya ufukweni, ‘inayokuja kwa kasi nchini’.    
    Messi anatakiwa ajitambue kwamba ana uwezo mkubwa na anaweza kuvuna fedha nyingi kutokana na kipaji chake- iwapo atazingatia miiko na maadili ya soka.
    Tafuta wakati wako, siku Arjen Robben anacheza akiwa amevaa jezi ya Bayern Munich au Uholanzi, angalia uchezaji wake halafu rejea uchezaji wa Messi wa Simba SC, kisha utajua thamani ya kinda huyo wa Wekundu wa Msimbazi.
    Robben anafahamika zaidi kwa umahiri wake wa kumiliki mpira na kupiga chenga za hatari, pamoja na kasi yake anapoteleza upande wa kulia wa Uwanja na kupiga mashuti na krosi nzuri ingawa anatumia mguu wa kushoto. Na Messi wa Simba SC, je unaweza kumsifia kwa lipi uwanjani kama si mambo kama hayo ya Robben?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UTAMSIFIA KWA LIPI RAMADHANI SINGANO ‘MESSI WA MSIMBAZI’? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top