• HABARI MPYA

    Thursday, January 02, 2014

    AZAM WAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI, WAWAFUMUA 2-0 ‘TIMU YA TAIFA’ YA UNGUJA

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC leo wameanza vyema michuano hiyo, baada ya kuifunga Spice Stars mabao 2-0 katika mchezo wa Kundi C jioni hii Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Hata hivyo, Azam ililazimika kusubiri kuanza kushangilia mabao yake dakika ya 71, baada ya mshambuliaji Mganda, Brian Umony kuwatoka mabeki wa Spice na kumchambua kipa Mohamed Silima, kufuatia pasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
    Wachezaji wa Azam FC wakimpongeza Brian Umony kushoto kwa kufunga bao la kwanza

    Brian aliyeingia dakika ya 59 kuchukua nafasi ya Muamad Ismael Kone, alikuwa mwiba wa safu ya ulinzi ya Spice.
    Himid Mao aliifungia Azam bao la pili dakika ya 86, baada ya kuuwahi mpira uliokuwa unaelekea mikononi mwa kipa Silima kufuatia shuti la Salum Abubakar na kupiga shuti lililotinga nyavuni.
    Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Mfaume Ali, mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcameroon Joseph Marius Omog kipindi cha pili kuwatoa Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Herman Tchetche na Kone na kuwaingiza Umony, Joseph Kimwaga na Seif Abdallah ndiyo yalileta ushindi huo.    
    Mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche akijiandaa kupiga krosi dhidi ya beki wa Spice Stars, Said Mussa 'Udindi'

    Azam walitawala zaidi mchezo katika dakika 45 za kwanza, lakini wakakosa mbinu za kuivunja ngome ya Spice, inayoundwa na wachezaji mchanganyiko wa Unguja.
    Kocha Omog alifanya mabadiliko kwenye kikosi cha kwanza cha Azam leo, akimrejesha Himid Mao kucheza nafasi ya kiungo pamoja na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Kipre Michael Balou, huku Erasto Nyoni akicheza beki ya kulia na Waziri Salum beki ya kushoto.
    Azam ilitawala sehemu ya kiungo na pasi nyingi ziliwafikia washambuliaji Kipre Herman Tchetche na Muamad Ismael Kone, lakini wakashindwa kabisa kufunga kipindi cha kwanza.
    Kwa ushindi huo, Azam inaongoza Kundi C kwa pointi zake tatu, na kubaki au kushuka itategemea na matokeo ya mchezo wa pili jioni ya leo Uwanja wa Amaan kati ya Ashanti United ya Dar es Salaam na Tusker FC ya Kenya.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Erato Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar, Muamad Kone/Brian Umony dk59, Kipre Tchetche/Seif Abdallah dk 70 na Khamis Mcha ‘Vialli’ dk49. 
    Spice Stars; Mohamed Silima, Abdallah Salum, Suleiman Ally/Abdulhakim Abdul dk81, Said Mussa, Said Ahmed, Hassan Said, Mohamed Salum, Mohamed Nassor/Yunus Bernad dk80, Ibrahim Hamad/Hakim Hamisi dk46, Abdallah Seif na Mohamed Abdulrahim. 
    Katika mchezo mwingine wa Kundi A, Uwanja wa Gombani, Pemba, URA  ya Uganda imetoka sare ya 2-2 na Chuoni ya Zanzibar.
    Mabao ya URA yamefungwa na Owen Kasuule dakika ya 44 na 57, wakati ya Chuoni yalifungwa na Shaaban Moke dakika ya 21 na Mwinyi Mngwali dakika ya 45 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM WAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI, WAWAFUMUA 2-0 ‘TIMU YA TAIFA’ YA UNGUJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top