• HABARI MPYA

    Wednesday, January 01, 2014

    HII NI AIBU YAO WENYEWE YANGA, MAPINDUZI DAIMA!

    KWA mara ya pili mfululizo, Yanga SC haitashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, kufuatia taarifa rasmi ya kujitoa kwake jana.
    Taarifa ya Yanga imesema kwamba uongozi wa klabu umewasilisha barua rasmi kwa ZFA (Chama cha Soka Zanzibar) kutoshiriki Kombe la Mapinduzi kutokana na kuamua kuvunja benchi nzima la Ufundi.
    Yanga imesitisha ajira za Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, kocha wa makipa, Razack Ssiwa na daktari wa timu, Nassoro Matuzya hivyo wanaungana na aliyekuwa bosi wao, Mholanzi Ernie Brandts aliyekuwa wa kwanza kuachishwa kazi kwa taarifa ya utangulizi siku 30 kabla kama wenzake.
     
    Kwa sasa uongozi wa Yanga upo katika mchakato wa kusaka warithi wa nafasi hizo haraka, ili waweze kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Taarifa hiyo pia imesema hadi sasa ni makocha 45 waliotuma maombi ya kazi na kwamba idadi hiyo imekuwa ikiongeza siku hadi siku. 
    Brandts amefukuzwa baada ya kuiongoza Yanga katika mechi 50, akiiwezesha kushinda mechi 29, sare 13 na kufungwa nane, akiwa anaiachia timu taji moja la ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita na msimu huu hadi sasa akiwa ameifanya timu hiyo iongoze Ligi Kuu baada ya mzunguko wa kwanza. 
    Mara ya mwisho Yanga SC kushiriki mashindano ya Mapinduzi ilikuwa ni mwaka 2011 ilipofungwa mabao 2-0 na Simba SC katika fainali, mabao ya Mussa Hassan Mgosi na Shijja Hassan Mkina, ambao tayari wamebaki historia Msimbazi.
    Mwaka jana, Yanga ilikuwa ina udhuru wa maana wa kutoshiriki mashindano, kwa sababu iliwenda kwenye ziara ya mafunzo Uturuki. Lakini hili la mwaka huu, yeyote atakayesikia sababu zilizotajwa anaweza kuangaliana usoni na mwenzake na kucheka kwa kejeli; “Wamewakimbia Simba”.
    Ndiyo, hilo ndilo wazo la haraka linaloweza kuja, hususan baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-1 na mahasimu wao hao wa jadi, Desemba 21, katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, ambao ndiyo uliosababisha kuvunjwa benchi la Ufundi.
    Ukweli ni kwamba, kitendo cha Yanga kujitoa kwenye mashindano hayo si cha kiunamichezo na pia hakizingatii historia ya klabu ya Yanga na Zanzibar.
    Makao makuu ya Yanga yapo Jangwani, ni kwa sababu ya lile jengo lake na Uwanja wa Kaunda na hiyo ndiyo alama na rasilimali pekee kubwa ya Yanga.
    Lile jengo la Jangwani lilijengwa kwa msaada mkubwa wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amaan Karume. Mwaka huu, Zanzibar inaazimisha miaka 50 ya Mapinduzi, yaliyoasisiwa na marehemu Karume, ambayo matunda yake ni Zanzibar huru.
    Katika sherehe muhimu, ambazo zitavutia viongozi wakuu wa nchi kadhaa barani, Yanga imealikwa na inajitoa kwa sababu nyepesi tu, bila kuzingatia mkono wa marehemu Karume ulivyochangia ustawi wa klabu yao.
    Sababu tumezisoma na tumezielewa, kweli timu haina benchi la Ufundi- lakini kitu ambacho unaweza kustaajabu ni kwamba, Yanga wana timu B, tena nzuri tu ambayo ina kocha wake, Salvatory Edward Augustino ‘Doctor’ aliyeiwezesha kufika fainali ya Kombe la Uhai, miezi miwili iliyopita michuano ya timu za vijana za wachezaji wa Ligi Kuu ya Bara.
    Kwa nini wasingeiandikia ZFA, pamoja na kuitaarifu mikasa ya kufukuza benchi zima la ufundi la kikosi cha kwanza, lakini pia wakaiomba badala yake, waruhusiwe kupeleka timu ya vijana, wakitolea mfano wapinzani wao wa jadi, Simba SC mwaka jana walipeleka timu yao ya vijana pia na ikafika hadi Nusu Fainali.
    Lakini kwa uongozi wa Yanga, jibu la haraka lilikuwa ni kuandika barua ya kujitoa. Hii ni fedheha kwa Yanga wenyewe, wanaonekana si wanamichezo na hawathamini mchango wa marehemu Karume na Wazanzibari kwa klabu yao. 
    Kombe la Mapinduzi litafanyika na litafana na siku ya kilele cha sherehe, Wazanzibari watapiga yowe la “Mapinduziii, daimaaa” na Yanga wanabaki na aibu yao. Heri ya mwaka mpya, Mungu atujaalie sote 2014 uwe mwaka mzuri kwetu. Amin. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HII NI AIBU YAO WENYEWE YANGA, MAPINDUZI DAIMA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top